JUMAMOSI JUMA LA 5 PASAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
Zab.119:33-40 V Kuomba maarifa
Ee Mungu, unioneshe kanuni zako,*
nami nitazishika mpaka mwisho.
Unieleweshe sheria yako,*
niishike kwa moyo wangu wote.
Uniongoze nishike amri zako,*
maana humo napata furaha.
Unipe ari ya kufuata sheria zako,*
sio tamaa ya kupata utajiri.
Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi;*
unifadhili kama ulivyoahidi.
Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako;*
ahadi unayowapa wanaokuheshimu.
Uniokoe na lawama ninazoogopa;*
maana hukumu zako ni safi.
Natamani sana kuzitii amri zako;*
unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.34 Sifa kwa wema wa Mungu
Mmeonja na kuona kuwa Bwana ni mwenye fadhili (1Pet.2:3)
I
Nitamtukuza Mungu nyakati zote,*
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.
Nitamwonea Mungu fahari,*
wanaodhulumiwa wasikie na wafurahi.
Mtukuzeni Mungu pamoja nami,*
sote pamoja tulisifu jina lake.
Nilimwomba Mungu, naye akanisikiliza,*
akaniondolea hofu zangu zote.
Mgeukieni Mungu, mpate kufurahi;*
hamtapata kamwe kusikitika.
Maskini alimlilia Mungu, naye akamsikiliza,*
na kumwokoa katika shida zake zote.
Malaika wa Mungu huwalinda wote wamchao,*
na kuwaokoa katika hatari.
Jioneeni wenyewe jinsi Mungu alivyo mwema.*
Heri wanaokimbilia usalama kwake.
Mcheni Mungu, enyi watakatifu wake;*
wenye kumcha hawakosi mahitaji yao.
Hata simba huona njaa kwa kutindikiwa;*
bali wanaomtii Mungu wana kila kitu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Njoni, enyi vijana, mkanisikilize,*
nami nitawafundisheni kumcha Mungu.
Je, wapenda kufurahia maisha;*
kuishi maisha marefu na ya fanaka?
Basi, acha kusema mabaya;*
achana na hila.
Jiepushe na uovu, utende mema;*
tafuta amani na kuizingatia.
Mungu huwaangalia waadilifu,*
na kusikiliza malalamiko yao;
lakini huwapinga watendao mabaya,*
awaondoa duniani, wasahauliwa kabisa.
Waadilifu wakimlilia Mungu, huwasikiliza,*
na kuwaokoa katika taabu zao zote.
Mungu yu karibu na waliovunjika moyo;*
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
Mateso ya mwadilifu ni mengi,*
lakini Mungu humwokoa katika yote.
Mungu humlinda mtu mwadilifu,*
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.
Ubaya utawaangamiza watu waovu;*
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.
Mungu atawaokoa watu wake, *
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Rom.5:10-11
Tulipokuwa bado adui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa
tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uzima wa Kristo. Wala si hayo
tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ametupatanisha
na Mungu.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: 1Kor.15:20-22
Ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka wafu, na ni uthibitisho kwamba wale waliolala
katika kifo watafufuliwa. Maana, kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo
hivyo nako kufufuka katika wafu kumesababishwa na mtu mmoja. Kama vile watu wote wanavyokufa
kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: 2Kor.5:14-15
Mapendo ya Kristo yanatumiliki sisi ambao tunatambua ya kwamba mtu mmoja tu amekufa kwa ajili
ya wote, na hiyo ina maana kwamba wote wanashiriki kifo chake. Alikufa kwa ajili ya watu wote,
ili wanaoishi wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa, akafufuliwa
kwa ajili yao.
K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.
SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi wa milele, ulitupatia uzima wa mbinguni kwa kuzaliwa kwetu upya katika
ubatizo; kwa neema yako, ulipanda ndani yetu mbegu ya umilele. Kwa maongozi yako utuongoze kwenye
utimilifu wa utukufu. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.