JUMAMOSI JUMA LA 5 PASAKA
MASOMO

SOMO: Mdo.16:1-10
Siku zile, Paulo alifika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike. Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.100:1-3,5(K)1
1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba;

(K) Mfanyieni Bwana shangwe dunia yote.

2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)

3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

SHANGILIO: Yn.20:29
Aleluya, aleluya,
Wewe Toma, umesadiki kwa kuwa umeniona,
wa heri wale wasioona wakasadiki.
Aleluya.

INJILI: Yn.15:18-21
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.

MAOMBI
Ulimwengu waweza kutuchukia sisi tunaosherekea ufufuko wa Bwana wetu pale tutakapofanya mambo yanayotushuhudia kuwa sisi si wa ulimwengu ingawa tumechaguliwa katika ulimwengu huu. Tuombe ili tuwe tayari kuvumilia tunapoudhiwa kwa ajili ya jina lake.

Kiitikio: Bwana utusikie, Bwana utusikilize.
1. Viongozi wote wa Kanisa lako wasichoke kuhimiza ushikaji wa amri zako na za Kanisa, pamoja na mapokeo hai tuliyorithishwa na mitume wako watakatifu.

2. Usimamie uhusiano mwema katika viongozi wa serikali na wa dini zenye nia njema kwa raia wao.

3. Wabatizwa wote tuisikie sauti ya Roho Mtakatifu anayetuongoza kwako na kutupatia nguvu ya kudumu katika utumishi wako mtakatifu.

4. Uwaweke ndugu zetu marehemu miongoni mwa wateule wako wanaotuombea daima.

Ee Mungu, ili kutukumbusha kwamba sisi tunaotimiza mapenzi yake tunaweza kutendewa na ulimwengu lolote lile ambalo yeye mwenyewe alitendewa, Mwanao amesema: “Mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake.” Utupatie nguvu na ari ya kuwa mashahidi wa Injili yako kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.