Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 5 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana amefufuka kweli, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!

Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!

Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!

Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534

2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ

3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.

Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876

4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.

Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.

Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.

Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.

Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.

Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.

Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.

Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7

5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.

Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.

Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.

Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.

Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750

7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.

Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.

Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.

Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.

Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695

ANT. I: Ee Bwana, unihuishe kwa upendo wako, aleluya.

Zab.119:145-152 XIX Kuomba usalama
Nakulilia kwa moyo wangu wote;/
unisikilize, Ee Mungu,*
nami nitazishika kanuni zako.

Nakusifu mara saba kila siku,*
nipate kuyashika mafundisho yako.

Asubuhi na mapema naamka niombe msaada;*
nitaitumainia kabisa ahadi yako.

Nakaa macho usiku kucha,*
ili niyatafakari maagizo yako.

Kwa upendo wako mkuu, Ee Mungu, unisikilize;*
uoneshe huruma yako, ukanisalimishe.

Wadhalimu wangu wakatili wanakaribia,*
watu ambao hawaishiki kamwe sheria yako.

Lakini wewe u karibu nami, Ee Mungu,*
na maagizo yako yote ni ya kuaminika.

Tangu zamani nimejifunza maagizo yako;*
wewe umeyaweka yadumu hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, unihuishe kwa upendo wako, aleluya.

ANT. II: Wale washindi, wimbo wa Musa, Mtumishi wa Bwana, ni wimbo wao; wimbo wa Mwana-kondoo ni wao, aleluya.

WIMBO: Kut.15:1-4a,8-13,17-18 Utenzi wa ushindi baada ya kuvuka Bahari ya Shamu
Wale waliomshinda yule mnyama waliimba wimbo wa Musa, Mtumishi wa Mungu (Ufu.15:2-3)

Nitamwimbia BWANA,*
kwa maana ametukuka sana;

Farasi na mpanda farasi *
amewatupa baharini.

BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu;*
Naye amekuwa wokovu wangu.

Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu;*
Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

BWANA ni mtu wa vita,*
BWANA ndilo jina lake.

Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini;*
Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa,

Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu,*
Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.

Adui akasema,/
Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara,*
Nafsi yangu itashibishwa na wao;

Nitaufuta upanga wangu,*
Mkono wangu utawaangamiza.

Ulivuma kwa upepo wako,*
bahari ikawafunikiza;

Wakazama kama risasi*
ndani ya maji makuu.

Ee BWANA, katika miungu*
ni nani aliye kama wewe?

Mtukufu katika utakatifu,/
Mwenye kuogopwa katika sifa zako,*
mfanya maajabu?

Ulinyosha mkono wako wa kuume,*
Nchi ikawameza.

Wewe kwa rehema zako/
Umewaongoza watu uliowakomboa,*
Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu.

Utawaingiza, na kuwapanda*
katika mlima wa urithi wako,

Mahali pale ulipojifanyia,*
Ee BWANA, ili upakae,

Pale patakatifu ulipopaweka imara,*
BWANA, kwa mikono yako.

BWANA atawala*
Milele na milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Wale washindi, wimbo wa Musa, Mtumishi wa Bwana, ni wimbo wao; wimbo wa Mwana-kondoo ni wao, aleluya.

ANT. III: Fadhili zake kwetu ni kuu, aleluya.

Zab.117 Kumsifu Mungu
Nawaambieni,.. nao watu wa mataifa mengine wamtukuze Mungu kwa sababu ya huruma yake (Rom.15:8-9)

Enyi mataifa yote, msifuni Mungu!*
Enyi watu wote, msifuni!

Upendo wake mkuu kwetu ni thabiti;*
na uaminifu wake wadumu milele!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Fadhili zake kwetu ni kuu, aleluya.

SOMO: Rom.14:7-9
Hakuna mtu ye yote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe; maana tukiishi, twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana. Maana Kristo alikufa, akafufuka ili apate kuwa Bwana wa wazima na wafu.

KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Kristo alikufa na akawa mzima tena, ili aimarishe utawala wake juu ya wazima na wafu, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Kristo alikufa na akawa mzima tena, ili aimarishe utawala wake juu ya wazima na wafu, aleluya.

MAOMBI
Kristo ni mkate wa uzima, na atawafufua siku ya mwisho wale wanaolishwa neno lake na mwili wake.
W. Bwana, utujalie amani na furaha.

Mwana wa Mungu, uliyefufuka kutoka wafu, wewe ndiwe Bwana wa uzima;
- uwabariki ndugu zetu wote, na ututakatifuze Sisi. (W.)

Wewe ni amani na furaha ya wote wanaokuamini;
- utusaidie tuweze kuishi kama watoto wa nuru, tukiufurahia ushindi wako. (W.)

Uwajalie waamini wako walioko duniani kuwa na imani zaidi na zaidi;
- ututie nguvu tuweze kuushuhudia ufufuko wako mbele ya watu. (W.)

Ulivumilia mateso makali, upate kuingia katika utukufu wa Baba;
- uyafute machozi yote, na uigeuze huzuni iwe furaha. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kwa mara nyingine tena, tumtukuze na kumwomba Baba kwa maneno ya Kristo mwenyewe, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, ulitupatia uzima wa mbinguni kwa kuzaliwa kwetu upya katika ubatizo; kwa neema yako, ulipanda ndani yetu mbegu ya umilele. Kwa maongozi yako utuongoze kwenye utimilifu wa utukufu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.