JUMAMOSI JUMA 5 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Eze.37:21-28
Bwana Mungu asema hivi: Tazama, nitawatwaa wana wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda,
nami nitawakusanya pande zote, na kuwaleta katika nchi yao wenyewe; nami nitawafanya kuwa taifa
moja katika nchi hiyo, juu ya milima ya Israeli; na mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote; wala
hawatakuwa tena mataifa mawili, wala hawatagawanyikana kuwa falme mbili tena, hata milele. Wala
hawatajitia uchafu tena kwa vinyago vyao, wala kwa vitu vyao vichukizavyo, wala kwa makossa yao
mojawapo; lakini nitawaokoa, na kuwatoa katika makao yao yote, ambayo wamefanya dhambi ndani yake,
nami nitawatakasa; basi watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Na mtumishi wangu, Daudi,
atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao wataenenda katika hukumu zangu,
na kuzishika amri zangu, na kuzitenda. Nao watakaa katika nchi niliyompa Yakobo, mtumishi wangu,
walimokaa humo, wao na watoto wao, na watoto wa watoto wao, milele; na Daudi, mtumishi wangu, atakuwa
mkuu wao milele.
Tena nitafanya agano la amani pamoja nao; litakuwa agano la milele pamoja nao; nami nitaweka na kuwazidisha,
na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami nitakuwa
Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Na mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, mimi niwatakasaye Israeli,
patakatifu pangu patakapokuwa katikati yao milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.31:10-13(K)10
1. Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa,
Litangazeni visiwani mbali;
Mkaseme: Aliyemtawanya Israeli atamkusanya,
Na kumlinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
Amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.
(K) Bwana anatulinda kama mchungaji
alindavyo kundi lake.
2. Watakuja na kuimba katika mlima Sayuni.
Wataukimbilia wema wa Bwana,
Nafaka, na divai, na mafuta,
Na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe. (K)
3. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
Na vijana na wazee pamoja;
Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
Nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao. (K)
SHANGILIO: Zab.95:8,9
Leo msifanye migumu mioyo yenu,
lakini msikie sauti yake Bwana.
INJILI: Yn.11:45-57
Wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Maria, na kuyaona yale aliyoyafanya Yesu, wakamwamini.
Lakini wengine wakaenda zao kwa Mafarisayo wakawaambia aliyoyafanya. Basi wakuu wa makuhani
na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi.
Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa
letu. Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui
neno lolote; wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa
zima. Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule,
alitabiri ya kwamba Yesu atakaufa kwa ajili ya taifa hilo, wala si kwa ajili ya taifa hilo tu;
lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja. Basi tangu siku
ile walifanya shauri la kumwua. Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati ya Wayahudi; bali
alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na
wanafunzi wake. Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; na wengi wakakwea toka mashambani kwenda
Yerusalemu kabla ya Pasaka, ili wajitakase. Basi wao wakamtafuta Yesu, wakasemezana hali wamesimama
hekaluni, Mwaonaje? Haji kabisa sikukuu hii? Na wakuu wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri
ya kwamba mtu akimjua alipo, alete habari, ili wapate kumkamata.
MAOMBI
Ndugu, Yesu aliuawa ili awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe pamoja. Kwa kuwa dhambi ndizo
zilizowafanya watoto hao watawanyike, tuombe: Ee Bwana Yesu twakuomba:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Utufanye sisi wafuasi wako wote tuwe kundi moja kama wewe ulivyo mmoja na Baba na Roho Mtakatifu. Ee Bwana.
2. Utunasue na mitego ya adui shetani, uabudu sanamu, unajisi na chochote kinachopingana na mpango wako
wa ukombozi. Ee Bwana.
3. Mataifa yote yakujue kuwa wewe ndiwe Bwana wao; ili ishara unazozifanya ziwaongoe, badala ya kuwa
kikwazo kwao. Ee Bwana.
4. Utumiminie baraka zako, ili Juma Kuu linalokuja litutakatifuze; tupate kuadhimisha mateso, kifo na ufufuko wako
kwa mioyo iliyotakata na kwa mapendo makuu. Ee Bwana.
Ee Bwana, wewe wataka tuokoke lakini wenye matata ni sisi tuliosongwa na malimwengu. Ufanye mioyo yetu ifanane
na Moyo wako Mtakatifu. Unayeishi na kutawala daima na milele. Amina.