JUMAMOSI JUMA 4 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Yer.11:18-20
Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa
kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri
kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke
katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye
haki ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia
wewe neno langu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.7:1-2,8-12(K)1
1. Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,
Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
Asije akaipapura nafsi yangu kama simba,
Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya.
(K) Bwana, Mungu wangu,
nimekukimbilia Wewe.
2. Bwana, unihukumu mimi,
Kwa kadiri ya haki yangu,
Sawasawa na unyofu nilio nao.
Ubaya wao wasio haki na ukome,
Lakini umthibitishe mwenye haki. (K)
3. Ngao yangu ina Mungu,
Awaokoaye wanyofu wa moyo.
Mungu ni mwamuzi mwenye haki,
Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. (K)
SHANGILIO: Lk.15:18
Nitaondoka,
nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia: Baba,
nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.
INJILI: Yn.7:40-52
Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko
halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa
Daudi? Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata,
lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. Basi wale watumishi wakawaendea wakuu
wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta? Wale watumishi wakajibu, Hajanena
kamwe mtu yeyote kama huyu anavyonena. Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika?
Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati
wamelaaniwa. Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), Je!
Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia,
Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.
MAOMBI
Baadhi ya Wayahudi walimtesa Mtumishi wa Bwana kwa sababu hawakumjua sawasawa, wala hawakutaka kuupokea ukweli
wake. Tuombe neema ya Mungu ili, kadiri Fumbo la Pasaka linavyozidi kukaribia, tuweze kuhesabiwa haki mbele yake.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Utegue mitego ya maadui dhidi ya Kanisa na viongozi wake; na utufunulie ukweli wako, ili tupate kuutangaza siku
zote kwa ushujaa.
2. Wewe utoaye hukumu ya haki, uwahurumie wote wanaodhulumiwa kwa sababu ya kuutetea ukweli wa Injili yako.
3. Uwabariki mahakimu, wasuluhishi na wazee wote wa baraza; wasimhukumu mtu bila ya kumsikiliza kwanza.
4. Utupe msukumo wa kupatana na wote tulio na kinyongo nao kabla ya kuishiriki karamu yako ya Pasaka.
Ee Baba msamehevu, Mwanao aliyachukua maovu yetu kwa upole kama kondoo apelekwaye machinjoni. Utujalie uvumilivu,
wema na upole; ili tushirikishwe uzima mpya pamoja na Kristo. Anayeishi na kutawala, daima na milele. Amina.