JUMAMOSI JUMA 34 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Dan.7:15-27
Mimi Danieli, roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha.
Nikamkaribia mmoja wa hao waliosimama karibu, nikamwuliza maana ya kweli ya hayo yote. Basi akaniambia,
akanijulisha tafsiri ya mambo hayo. Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wane watakaotokea
duniani. Lakini watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam
hata milele na milele. Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wanne, aliyekuwa mbali na wenziwe
wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula,
na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na habari za zile pembe kumi
zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe
tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa
hodari kuliko wenzake. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda;
hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake. Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia
watakatifu waumiliki ufalme. Akanena hivi, Huyo mnyama wanne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia,
utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande
vipande. Na habari za zile pembe kumi katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine
ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.
Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye
ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na
nusu wakati. Lakini hukumu itawekwa, nao watamwondolea mamlaka yake, kuyapoteza na kuyaangamiza,
hata milele. Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa
watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia
na kumtii.
WIMBO WA KATIKATI: Dan.3:82-87 (K)59
1. Wanadamu, mhimidi Bwana;
Msifuni na kumwadhisha milele.
Bani Israeli, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni na mwadhimisha milele.
2. Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Watumishi wa Bwana mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele. (K)
3. Roho na nafsi zao wenye haki mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni,
Mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele. (K)
SHANGILIO: Yak.1:18
Aleluya, aleluya!
Kwa kupenda kwake mwenyewe,
Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli,
tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya!
INJILI: Mk1:14-20
Yesu aliwambia wanafunzi wake: Jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na
masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo
itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati,
mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, leo tunapoelekea mwishoni kabisa mwa mwaka huu wa kiliturujia, tunajikabidhi
mikononi mwa Mama Bikira Maria huku tukikushukuru.
Kiitikio: Upokee shukrani zetu.
1. Kwa kuwa umetujalia viongozi wa Kanisa, ambao wanajitahidi kukutumikia Wewe na
Kanisa lako kadiri wawezavyo. Ee Bwana.
2. Kwa kuwa viongozi na watawala wote wenye nia njema wameonesha juhudi za kutetea
uhuru, haki na amani ya kweli. Ee Bwana.
3. Kwa kuwa sisi sote umetulisha neno lako na kutuandaa kwa hukumu ya siku ya
mwisho. Ee Bwana.
4. Kwa kuwa umekuwa ukikaa kwetu katika Ekaristi Takatifu na kwa namna nyingine
nyingi; na umetuahidi kuja tena upesi. Ee Bwana.
5. Kwa kuwa marehemu wetu wengi wanasamehewa dhambi zao na kupewa uzima wa
milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetuagiza kukesha kila wakati tukiomba bila kuchoka, upokee
maombi na shukrani zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.