JUMAMOSI JUMA 33 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Mak.6:1:13
Mfalme Antioko alipokuwa akisafiri katika nchi za juu alisikia habari za Elimaisi, mji wa Uajemi,
uliosifiwa sana kwa utajiri wake, fedha yake na dhahabu yake. Hekalu lake lilikuwa na mali nyingi,
na humo mlikuwa na ngao za dhahabu, na dirii, na silaha za vita ambazo ziliwekwa humo na Iskanda,
mwana wa Filipo, mfalme wa Makedonia aliyekuwa wa kwanza kuwatawala Wayunani. Basi, alifika huko,
akitaka kuutwaa mji na kuuteka nyara. Lakini haikuwezekana, kwa sababu shauri lake lilijulikana kwa
watu wa mjini, wakajipanga kufanya vita naye. Akakimbia, akaondoka kwa moyo mzito kurudi Babeli.
Akaletewa habari huko Uajemi ya kuwa majeshi waliokwenda kuipiga nchi ya Uyahudi wameshindwa; tena
Lisia, aliyekwenda kwao na jeshi la nguvu sana, alikimbizwa mbele yao; nao wamepata nguvu nyingi
kwa sababu ya silaha na zana za vita na nyara walizoziteka kwa majeshi waliyoyashinda. Zaidi ya hayo,
wamelibomoa lile chukizo alilolijengesha juu ya madhabahu Yerusalemu, na kupazungusha patakatifu kuta
ndefu, kama zamani, na mji wake Bethsura pia. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno hayo, alishikwa na
bumbuazi akafadhaika mno. Akakaa huko siku nyingi, maana alilemewa na huzuni nyingi hata alidhani
atakufa. Akawaita rafiki zake wote, akawaambia, Usingizi umefarakana na macho yangu, hata moyo
wangu umevunjika kwa taabu. Nasema ndani yangu, Jinsi nilivyosibiwa! Ninazama katika maji mengi!
Katika enzi yangu nalikuwa mstahiki, mwenye kupendwa. Lakini sasa nayakumbuka mabaya niliyoyafanya
Yerusalemu, jinsi nilivyovichukua vyombo vyote vya fedha na dhahabu vilivyokuwapo, na kupeleka majeshi
kuwaharibu wenyeji wa Yerusalemu bila sababu. Nafahamu ya kuwa kwa sababu hiyo maovu haya yamenipata,
hata, tazama, ninakufa kihoro katika nchi ya kigeni.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.9:1-2,5,15,18 (K)15
1. Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote;
Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;
Nitafurahi na kukushangilia Wewe;
Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu.
(K) Nitaufurahia wokovu wako, Ee Bwana.
2. Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma;
Hujikwaa na kuangamia mbele zako.
Umewakembea mataifa;
Na kumwangamiza mdhalimu;
Umelifuta jina lao milele na milele. (K)
3. Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya;
Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao.
Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima;
Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele. (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu,
awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!
INJILI: Lk.20:27-40
Baadhi ya masadukayo, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, walimwendea Yesu, wakamwuliza,
wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini
hana mtoto, na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa
kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto; hata wa
tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye.
Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana
wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu
ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu
huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa
wafu hufufuliwa, hata na Musa alionesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni
Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio
hai; kwa kuwa wote huishi kwake. Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema;
wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu wa walio hai, kwa maombezi ya Bikira Maria, sisi tulio hai hapa duniani
twaja mbele yako na maombi yetu tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uzidi kutufunulia Fumbo Kuu la Pasaka kwa njia ya Maandiko matakatifu na mafundisho
ya Wachungaji uliowatuma kwetu. Ee Bwana.
2. Wakuu wa nchi zote duniani wasimamie haki na uhuru wa dini inayokubalika mbele zako;
ili watangazaji wa neno lako waende popote kwa usalama na bila hofu yoyote. Ee Bwana.
3. Ulilinde Kanisa lako Takatifu Katoliki dhidi ya maadui wanaotaka kuliharibu au
kulivunjia umoja wake uliopo. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote kuona huzuni kwa makosa tunayofanya kutokana na udhaifu wetu
wa kibinadamu, na utujalie toba na mapatano ya kweli. Ee Bwana.
5. Uwapokee marehemu wetu, wapate kuishi pamoja nawe na watakatifu wako
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu ambaye kwako wote huishi, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.