JUMAMOSI JUMA 32 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Hek.18:14-16,19:6-9
Mambo yote yalipokuwa kimya, na usiku ulikuwa katikati ya mwendo wake mwepesi, Neno lako Mwenyezi
alishuka mbinguni kutoka kiti chako cha kifalme, shujaa aliye hodari, katika nchi iliyoposishwa
hukumu, mwenye upanga mkali, ndio amri yako isiyopindika, akasimama na kujaza mambo yote mauti,
na pindi alipogusa mbingu akaikanyaga nchi. Kwa maana ulimwengu mzima, kwa kadiri ya asili yake,
ulifanyika tena mpya, kwa kuzitii amri zako hizi na hizi, ili watoto wako walindwe wasipate dhara.
Uwingu ulionekana uliokitia uvuli kituo chao, nan chi kavu ikapanda kutoka pale palipokuwapo maji
kwanza, katika Bahari ya Shamu kukawa barabara isiyo na zuio, na uwanda wenye majani katika mawimbi
yaumkayo. Hapo watu wako wakapita pamoja na majeshi yao yote, ambao kwa mkono wako walifunikwa,
wakiisha kuona maajabu makuu. Wakazunguka-zunguka huru kama farasi, wakaruka-ruka kama wana-kondoo,
wakikuhimidi Wewe, Bwana, uliyekuwa mkombozi wao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:2-3,36-37,42,43 (K)5
1. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.
2. Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi.
Malimbuko ya nguvu zao.
Akawatoa hali wana fedha na dhahabu,
Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa. (K)
3. Maana alilikumbuka neno lake takatifu,
Na Ibrahimu, mtumishi wake.
Akawatoa watu wake kwa shangwe,
Na wateule wake kwa nyimbo za furaha. (K)
SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya!
Neno lako ni taa ya miguu yangu,
na mwanga wa njia yangu.
Aleluya!
INJILI: Lk.18:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate
tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji Fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika
mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui
wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali
watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia
daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule
wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini,
atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona Imani duniani?
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu aliyewakomboa Waisraeli utumwani
Misri kwa mkono wa Musa, ndiye aliyetukomboa sisi
toka utumwa wa dhambi kwa njia ya Mwanae Yesu
Kristo. Kwa maombezi ya Bikira Maria, tumwombe.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ubariki juhudi za Maaskofu na Wakleri wote katika
kuhubiri toba iletayo msamaha wa dhambi kwa watu
wako. Ee Bwana.
2. Uwe pamoja na viongozi wetu wa serikali ili, hata
wafanyapo mikataba na watu wa mataifa mengine,
wazilinde mila na desturi zetu njema; tupate kuwa
watenda kazi pamoja na kweli. Ee Bwana.
3. Matukio ya kihistoria yanayoonesha nguvu yako kuu
dhidi ya yule mwovu na upendo wako mkuu kwa watu
wako, yawe kichocheo cha wongofu wa watu
wengi. Ee Bwana.
4. Utuongezee ari ya kusali bila kuchoka na udumifu
katika kutenda mema tukisukumwa na upendo kwako
na kwa wenzetu. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wasamehewe dhambi zao na
kufikishwa huko uliko Wewe. Ee Bwana.
Ee Mungu unayewapatia haki wanaokulilia, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.