JUMAMOSI JUMA 31 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.16:3-9,16,22-27
Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu; waliokuwa tayari hata
kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa
ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao. Nisalimieni Epaineto,
mpenzi wangu, aliye malimbuko ya Asia kwa Kristo. Nisalimieni Mariamu, aliyejitaabisha sana kwa
ajili yenu. Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu
miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika Kristo kabla yangu. Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu
katika Bwana. Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika Kristo, na Stakisi, mpenzi wangu.
Salimianeni kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo wawasalimu. Mimi Tertio, niliyandika waraka
huu, nawasalimu katika Bwana. Gayo, mwenyeji wangu na wa Kanisa lote pia awasalimu. Erasto, wakili
wa mji, awasalimu, na Kwarto, ndugu yetu. Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa
na injili yangu na kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo na ile amri iliyositirika tangu
zamani za milele, ikadhihirishwa wakati huu kwa maandiko ya manabii ikajulikana na mataifa yote
kama alivyowaamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani. Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu
una yeye kwa Yesu Kriso, milele na milele. Amina.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:2-5,10-11 (K)1
1. Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,
Wala ukuu wake hautambulikani.
(K) Nitalihimidi jina lako milele, Ee Bwana.
2. Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yake,
Kitayatangaza matendo yake makuu.
Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako,
Na matendo yako yote ya ajabu. (K)
3. Ee Bwana, kazi zako zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako. (K)
SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana,
ututakase kwa ile kweli.
Aleluya!
INJILI: Lk.16:9-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana
wawakaribishe katika makao ya milele. Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu
katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa
pia. Bali, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali
ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu
wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu au
kumpenda huyu, ama atamshikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, sasa tumpelekee Mungu maombi yetu. Ee Mungu,
kwa maombezi ya Bikira Maria, twakuomba.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Maaskofu na Mapadre wote wafanywe imara
katika kuihubiri Injili, ili mataifa yote waijue na
kuitii imani ya kweli. Ee Bwana.
2. Kila mwenye wajibu wa kutoa huduma kwa jamii
yoyote ile halali ajaliwe uaminifu katika mambo yote,
madogo na makubwa. Ee Bwana.
3. Utuepushe na tamaa mbaya, dhihaka na tabia ya
kujidai haki mbele ya wenzetu, ili Wewe utukuzwe. Ee Bwana.
4. Utujalie moyo wa sadaka kwa wenye shida; kwani
sote twajua kudhiliwa na kufanikiwa na katika hali na mambo
yoyote, umetufundisha kushiba na kuona njaa; kuwa na vingi
na kupungukiwa. Ee Bwana.
5. Uwaepushe marehemu wetu na laana ya milele na
kuwaingiza mbinguni kunako uzima wa milele. Ee Bwana.
Ee Mungu uijuaye mioyo ya watu, uyapokee maombi
yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.