JUMAMOSI JUMA 29 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.8:1-11
Hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule
ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana
kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe
katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili;
ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali
mambo ya roho. Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao
roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.
Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi
kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani
yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo,
huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu
i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani
yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa,
kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1-6 (K)6
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Ndicho kizazi cha wakutafutao uso wako,
Ee Bwana.
2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)
3. Atapokea baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
SHANGILIO: Kol.3;16,17
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika yote.
Mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya!
INJILI: Lk.13:1-9
Wakati huo walikuwapo watu waliompasha Yesu habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya
damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye
dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu,
ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu,
ukawaua mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia,
Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa
na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafua matunda juu yake, asipate.
Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu
ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache
mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa,
ndipo uukate.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kama vile mti usivyoweza kuzaa matunda
usipotunzwa vizuri, ndivyo sisi tusivyoweza kuokoka
bila kuacha mabaya na kutenda mema. Tuombe neema
ya Mungu.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Kwa maombezi ya Mama yetu Bikira Maria, uwatie
moyo viongozi wetu wa Kanisa, katika juhudi
zao za kuwahimiza watu watubu na kuiamini
Injili. Ee Bwana.
2. Uwajalie viongozi wa taasisi au jamii zetu na wote
wenye mwili kukumbuka kuwa nia ya mwili ni mauti;
bali nia ya roho ni uzima na amani. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote kutowahukumu wengine, na badala
yake tuwatangazie Injili kwa mfano wa maisha ya
toba na mapendo ya kweli. Ee Bwana.
4. Waliokumbwa na malimwengu wasiyumbishwe na
kila upepo wa elimu, kwa hila, ujanja, au
udanganyifu; bali watumie vipawa ulivyowajalia,
waishike kweli na kuufikia ukamilifu. Ee Bwana.
5. Uzijalie uzima na amani huko mbinguni roho za ndugu
zetu marehemu. Ee Bwana.
Ee Mungu uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya huyo
Kristo Bwana wetu. Amina.