JUMAMOSI JUMA 27 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Yoe.3:12-21
Bwana asema hivi: Mataifa na wajihimize, wakapande juu katika bonde la Yehoshafau; maana huko ndiko
nitakakoketi niwahukumu mataifa yote yaliyo pande zote. Haya! Utieni mundu, maana mavuno yameiva;
njoni, kanyageni; kwa maana shinikizo limejaa, mapipa nayo yanafurika; kwani uovu wao ni mwingi sana.
Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya Bwana i
karibu, katika bonde la kukata maneno. Jua na mwezi vimetiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza. Naye
Bwana atanguruma toka Sayuni, atatoa sauti yake toka Yerusalemu; na mbingu na nchi zitatetemeka;
lakini Bwana atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome ya wana wa Israeli. Hivyo ndivyo mtakavyojua
ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, nikaaye Sayuni, mlima wangu mtakatifu; ndipo Yerusalemu
utakapokuwa mtakatifu, wala wageni hawatapita tena ndani yake kamwe. Tena itakuwa siku ile, ya
kwamba milima itadondoza divai tamu, na vilima vitatiririka maziwa, na vijito vyote vya Yuda vitatoa
maji tele; na chemchemi itatokea katika nyumba ya Bwana, na kulinywesha bonde la Shitimu. Misri
itakuwa ukiwa, na Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya dhuluma waliowatenda wana wa Yuda; kwa
sababu wamemwaga damu isiyo na hatia katika nchi yao. Bali Yuda atadumu milele, na Yerusalemu tangu
kizazi hata kizazi. Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana Bwana ndiye akaaye Sayuni.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.97:1-2,5-6,11-12 (K)12
1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.
2. Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake. (K)
3. Nuru imemzukia mwenye haki,
Na furaha wanyofu wa moyo.
Enyi wenye haki, mmfurahieni Bwana,
Na kulishukuru jina lake takatifu. (K)
SHANGILIO: Zab.25:4,5
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana, unijulishe njia zako,
unifundishe mapito yako.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:27-28
Ikawa, Yesu alipokuwa akisema, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia
Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao
neno la Mungu na kulishika.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu ni kimbilio letu na ngome yetu.
Walisikiao neno lake na kulishika ndio wenye heri.
Tumwombe Mungu kupitia Mama yetu Bikira Maria.
tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Askofu wetu F. na Mapadre wetu wote wazidi kuwa
madhubuti kimwili na kiroho, wapate kuwaimarisha
watu wao katika imani na mapendo kwako. Ee Bwana.
2. Uwe pamoja na viongozi wetu wa serikali
wanaolisikia neno lako na kulishika; na uwahesabie
haki kwa imani, wapate kuwa warithi sawasawa na
ahadi yako kwa wakuaminio. Ee Bwana.
3. Watu wote duniani wajaliwe kujiandaa kwa ajili ya
siku yako ya hukumu ambayo unaifahamu Wewe tu. Ee Bwana.
4. Uwabariki wazazi wetu na utujalie kuutetea uhai
wetu na wa wenzetu, wakubwa kwa wadogo, kama
neno lako linavyotuamuru. Ee Bwana.
5. Uwahurumie ndugu zetu marehemu na kuwapa furaha
isiyo na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, uliyependa Bikira Maria apewe heri kufuatia
matendo makuu ya Mwanao, uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.