JUMAMOSI JUMA 26 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Bar.4:5-12,27-29
Jipeni moyo watu wangu, Israeli mnaokumbukwa! Mliuzwa kwa mataifa lakini hamkuangamia. Kwa kuwa
mlimtia Mungu ghadhabu mlitolewa kwa adui zenu; Mlimwasi yeye aliyewaumba, mkitoa sadaka kwa pepo,
si kwa Mungu; mlimsahau Mungu wa milele aliyewalea, na Yerusalemu mama yenu. Huyu mama aliiona
ghadhabu ya Mungu iliyokuja juu yenu, akasema: Enyi wa Sayuni, sikilizeni! Mungu ameleta juu yangu
huzuni kubwa. Nimeuona utumwa wa wanangu ambao Aliye wa Milele amewapatiliza. Kwa furaha naliwalea;
bali kwa kilio na maombolezo naliwaaga. Asisimange juu yangu mtu ye yote, mimi niliye mjane na
kuachwa na watu. Kwa sababu ya dhambi za wanangu nimeachwa ukiwa, kwa kuwa walikengeuka na kuiacha
sheria ya Mungu. Jipeni moyo, wanangu, mlilieni Mungu! Maana yeye aliwapatiliza mambo haya atawakumbuka.
Kama ilivyokuwa nia yenu kumwasi Mungu, rudini sasa, mtafuteni mara kumi zaidi; maana yeye aliyeyaleta
mapigo haya juu yenu atawarudishia Furaha ya milele pamoja na wokovu wenu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.69:32-36 (K)33
1. Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mumtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafungwa wake.
Mbingu na nchi zimsifu,
Bahari na vyote viendavyo ndani yake.
(K) Bwana huwasikia wahitaji.
2. Maana Mungu ataiokoa Sayuni,
na kuijenga miji ya Yuda,
Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki.
Wazao wa watumishi wake watairithi,
Nao walipendao jina lake watakaa humo. (K)
SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Yesu akamjibu,
“Mtu akinipenda atashika neno langu,
na Baba yangu atampenda,
nasi tutakuja kwake na kukaa naye.
Aleluya!
INJILI: Lk.10:17-24
Wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia,
Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka
na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile
pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. Saa ile ile alishangilia
kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya
umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo
ilivyokupendeza. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba;
wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Akawageukia wanafunzi
wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba
manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia
ninyi wasiyasikie.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu wapendwa, Mungu yupo tayari kuwasamehe
wale wanaomnyenyekea na kutubu. Ndio wale wanaofananishwa
na watoto wachanga. Tuombe msaada wake tunaposali.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Kwa maombezi ya Bikira Maria, viongozi wetu wa
Kanisa wazidi kuwapa moyo waliokata tamaa ya
maisha kwa sababu mbali mbali, na kuwafariji kwa
neno lako la wokovu. Ee Bwana.
2. Uzidi kuubarikia uongozi wa Raisi wetu zaidi ya
mwanzo wake, apate kuzitimiza ndoto zake za
kulijenga taifa letu katika nyanja zote muhimu. Ee Bwana.
3. Umwangushe shetani na kutuepusha na kitu chochote
chenye kutudhuru, tupate kutimiza mapenzi yako kwa
amani na utulivu. Ee Bwana.
4. Uzipatilize adhabu tulizostahili kwa makosa yetu, na
utupe hekima na nguvu ya kumshinda yule mwovu. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu furaha ya milele na
kuyaandika majina yao huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.