JUMAMOSI JUMA 25 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Zek.2:1-5,10-11
Niliinua macho yangu, nikaona, na tazama, mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake. Ndipo nikasema,
unakwenda wapi? Akaniambia, Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione upana wake ulivyo na urefu wake
ulivyo. Na tazama, yule malaika aliyesema nami akasimama karibu, na malaika mwingine akatoka ili
kuonana naye; naye akamwambia, Piga mbio, kamwambie kijana huyu, na kusema, Yerusalemu utakaliwa
na watu, kama vijiji visivyo na kuta, kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo ndani yake.
Kwa maana mimi, asema Bwana, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa ukuta
wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakaa, kati yako, asema Bwana. Na mataifa mengi watajiunga
na Bwana katika siku ile, nao watakuwa watu wangu.
WIMBO WA KATIKATI: Yer.31:10-13 (K)10
1. Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa,
Litangazeni visiwani mbali, mkaseme,
Aliyemtawanya Israeli atamkusanya,
Na kumlinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
2. Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
Amemkomboa mkononi mwake
aliyekuwa hodari kuliko yeye. (K)
3. nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni,
wataukimbilia wema wa Bwana,
nafaka, na divai, na mafuta,
na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe.
Na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji,
Wala hawatahuzunika tena kabisa. (K)
4. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
Na vijana na wazee pamoja.
Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
Nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao. (K)
SHANGILIO: Zab.19:8
Aleluya, aleluya!
Sheria za Bwana ni sawa, huufurahisha moyo;
amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi, humwelimisha mtu.
Aleluya!
INJILI: Lk.9:43-45
Makutano walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake,
Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono
ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza
maana yake neno lile.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu alipenda kumtukuza Mwanae Yesu Kristo
hapa duniani kwa namna mbali mbali. Pamoja na
Bikira Maria, tumpelekee Mungu maombi yetu:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umwongezee Baba Mtakatifu F. na viongozi wote
wa Kanisa ujasiri katika kuyatetea mafumbo makuu
ya imani yetu wakati wote na katika mazingira yoyote. Ee Bwana.
2. Ulikinge Kanisa lako na hila za wanaompinga Kristo
wako, tupate kuepukana na maasi na kuuona utukufu
wa Mwanao kati yetu. Ee Bwana.
3. Utuongezee imani juu ya uwepo wako kati yetu
katika neno lako, katika Sakramenti na katika
wenzetu; na utuondolee hofu na mahangaiko. Ee Bwana.
4. Vijana wote wakukumbuke Wewe muumba wao
wakati bado wanaufurahia ujana wao; ili matendo
yao mema yakubalike siku ya hukumu. Ee Bwana.
5. Uwaite ndugu zetu marehemu wapate kuishi pamoja
nawe milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.