JUMAMOSI JUMA 24 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Tim.6:13-16
Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama
maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato, kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama,
hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye
aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana; ambaye yeye peke yake
hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kuharibiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala
awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina
WIMBO WA KATIKATI: Zab.100 (K)2
1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.
(K) Njoni mbele za Bwana kwa kuimba.
2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
3. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K)
4. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
SHANGILIO: Kol.3:16,17
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristo
likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote;
mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya!
INJILI: Lk.8:4–15
Mkutano mkuu ulipokutanika, na wale waliotoka kila mji wakimjia, Yesu alisema kwa mfano: Mpanzi
alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia,
zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila. Nyingine zikaanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka
kwa kukosa rutuba. Nyingine zikaanguka kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga.
Nyingine zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia. Alipokuwa akinena hayo
alipaza sauti akisema, Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie. Wanafunzi wake wakamwuliza, Maana
yake nini mfano huo? Akasema, Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa
mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe. Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni
neno la Mungu. Wale wa karibu na njia ndio wasikiaopo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana
mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga. Na zilipoanguka penye miiba ni
wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya,
wasiivishe lolote. Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao
hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, pamoja na vipaji vingi tulivyopewa, bado tunahitaji
neema ya Mungu. Ee Mungu, kwa maombezi ya
Bikira Maria, twakuomba.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Askofu wetu F. na Mapadre wote wajaliwe ari ya
kubuni mbinu zaidi za uinjilishaji. Ee Bwana.
2. Tunawaombea viongozi wa serikali, ili wapandikize
mioyoni mwa watu sera zenye nguvu ya
kuondoa uharibifu na kujenga maadili mema. Ee Bwana.
3. Ulikinge Kanisa lako na maadui wanaolisonga na
kulipiga vita ili, kwa msaada na neema yako, Injili
yako iweze kuhubiriwa na kuenea duniani kote. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote kujitayarisha vema kabla ya kulisoma
au kulisikiliza neno lako; lipate kukaa ndani
ya mioyo yetu na kuzaa matunda bora. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wakaribishwe kwako Wewe
usiyepatikana na mauti. Ee Bwana.
Ee Mungu, unayekaa katika nuru isiyoweza kuharibiwa,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.