JUMAMOSI JUMA 22 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kol.1:21-23
Ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya,
amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake,
watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi,
mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika
viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nalikuwa mhudumu wake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.54:1-2,4,6 (K)4
1. Ee Mungu, kwa jina lako uniokoe,
Na kwa uweza wako unifanyie hukumu.
Ee Mungu, uyasikie maombi yangu,
Uyasikilize maneno ya kinywa changu.
(K) Mungu ndiye anayenisaidia.
2. Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia;
Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu. (K)
3. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu;
Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema. (K)
SHANGILIO: Zab.119:34
Aleluya, aleluya!
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:1-5
Ilikuwa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja
masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao. Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia,
Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato? Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo
alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? Jinsi alivyoingia katika
nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si
halali kuila ila kwa makuhani peke yao. Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, tumwombe Mungu kwa maombezi ya Bikira
Maria mama yetu tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Askofu wetu F. na Mapadre wote wadumu katika
kulihubiri neno lako na kuumega mkate, ili watu
wako wapate daima kushibishwa kwa mema yako. Ee Bwana.
2. Viongozi wetu wa serikali wawapiganie wanaowahudumia
watu wako katika mazingira magumu,
ili wapate unafuu wa maisha. Ee Bwana.
3. Uingilie kati vita na dhuluma vilivyo dhidi ya watu
wasio na hatia, ili amani itawale na waamini wako
wakuabudu kwa utulivu. Ee Bwana.
4. Uwajalie wakristo wote kuikiri imani kwa imara ya
kudumu, wakifuata mashauri ya Injili yenye tumaini
la kweli. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wajaliwe amani isiyo na kikomo
huko juu mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetupatanisha ili tuwe watakatifu bila
mawaa, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.