JUMAMOSI JUMA 21 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1The.4:9-12
Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.
Kwa maana mnafanya neno hili kwa ndugu wote walio katika Makedonia yote. Lakini twawasihi, ndugu,
mzidi sana. Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe,
kama tulivyowaagiza; ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu chochote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1,7-9 (K)9
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umetendea wokovu.
(K) Atawahukumu mataifa kwa adili.
2. Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
Mito na ipige makofi,
Milima na iimbe pamoja kwa furaha.
Mbele za Bwana;
Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)
3. Atahukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa adili. (K)
SHANGILIO: Zab.25:4,5
Aleluya, aleluya!
Mungu alikuwa ndani ya Kristu,
akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake,
ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya!
INJILI: Mt.25:14-30
Yesu aliwaelezea wanafunzi wake mfano huu: Mtu aliyetaka kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka
kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila
mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya
biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye
akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha
fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.
Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka
kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia,
Vema, mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia
katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka
kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia,
Vema mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia
katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua
ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; basi nikaogopa, nikaenda
nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia,
wewe mtumwa mbaya na ulegevu, ulijua yakuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi,
ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.
Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. Kwa maana kila mwenye kitu
atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alichonacho atanyang’anywa. Na
mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu amewekeza kwa kila mmoja wetu talanta
kadhaa, zipate kuzaa faida. Kwa vile uzalishaji faida
iliyotarajiwa unasongwa na vikwazo vingi, tuombe.
Kiitikio: Usikie sala yetu.
1. Kwa maombezi ya Bikira Maria, viongozi wetu wa
Kanisa wazidi kuhamasisha roho ya uwajibikaji, ili
kuzitegemeza familia na Kanisa zima. Ee Bwana.
2. Kwa kuwa “Si wengi wenye cheo walioitwa,”
uwajalie viongozi wetu wa serikali kuwateua watu
waadilifu na wenye hekima itokayo kwako, wapate
kuwaongoza na kuwatetea wanyonge. Ee Bwana.
3. Uwajalie wote wenye mali kukumbuka kuwa vyote
walivyo navyo vyatoka kwako; na siku ya mwisho
watapaswa kutolea hesabu mbele yako. Ee Bwana.
4. Sisi sote tujaliwe utulivu, tupate kutimiza wajibu zetu
kama tulivyoagizwa; na hivi kuwa mfano bora kwa
wenzetu na kujipatia riziki na unafuu wa maisha kwa
njia halali. Ee Bwana.
5. Uwaingize marehemu wetu katika furaha yako Wewe,
Bwana wao waliyekutumaini siku zote. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.