JUMAMOSI JUMA 20 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rut.2:1-3,8-11;4:13-17
Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa
Boazi. Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake
yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. Basi akaenda, akaja
akaokota masazo kondeni nyumba ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya
shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. Basi Boazi akamwambia
Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba liongine, wala usiondoke hapa,
lakini papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao;
je! Sikuwaagiza vijana wasikuse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyotenda hao
vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machozi pako,
hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia
mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa,
ukafikilia watu usiowajua tangu hapo. Basi Boazi akamtwaa ruthu, naye akawa mke wake; naye akaingia
kwake; na Bwana akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa motto wa kiume. Nao wale wanawake wakamwambia
Naomi, Na ahimidiwe Bwana, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe
kuu katika Israeli. Naye atakurejezea uhai wako, na ambaye akupenda, naye anakufaa kuliko watoto mtoto,
akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake. Nao wale wanawake waliokuwa jirani zake wakampa jina, wakisema,
Naomi amezaliwa mwana; wakamwita jina lake Obedi; yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.128:1–5 (K)4
1. Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
(K) Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
2. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako. (K)
3. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni;
Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako. (K)
SHANGILIO: Zab.119:28,33
Aleluya, aleluya!
Unitie nguvu sawasa na neno lako, ee Bwana,
unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya!
INJILI: Mt.23:1–12
Yesu aliwambia makutano na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti
cha Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao,
msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani
mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na
watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu,
na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi
msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani;
maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja,
naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza, atadhiliwa;
na yeyote atakayejidhili, atakwezwa.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu wapendwa, sisi sote tunaye Mwalimu mmoja,
Baba mmoja na Kiongozi mmoja tu. Na hivi tumwombe
kwa unyenyekevu.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Wote wenye Daraja Takatifu za Kanisa wajaliwe
kukuhubiri Wewe Mungu kwa makini zaidi, ili
wasikilizaji wao wamjue nani aliye Mwalimu, Baba
na Kiongozi wao wa kweli. Ee Bwana.
2. Uwaepushe na unafiki wa kifarisayo viongozi wetu
wote, ili wayatende yale wanayoyasema kwa ustawi
wa jamii zao zinazowategemea. Ee Bwana.
3. Utujalie sisi sote unyenyekevu na ukarimu kwa wageni
na wote wenye shida ili, katika hao wahitaji, tukutane
nawe na kupata tuzo la wenye haki. Ee Bwana.
4. Uiguse mioyo ya waliokusahau; wapate kurudi
kanisani na kuuona utukufu wako na kiti chako cha
enzi. Ee Bwana.
5. Uwakaribishe ndugu zetu marehemu kwenye makao
yako ya kudumu huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayempa akuombaye, uyapokee maombi
yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.