JUMAMOSI JUMA 19 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Yos.24:14-29
Yoshua aliwaambia makutano: Sasa mcheni Bwana, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka
mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye Bwana.
Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu
ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa
katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana. Hao watu wakajibu wakasema, Hasha!
Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha
sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile
kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa
yote tuliopita katikati yao. Bwana ndiye aliyewafukuza watu wa mataifa yote watoke mbele yetu, naam,
Waamori waliokaa katika nchi hii; asi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia Bwana; maana yeye ndiye
Mungu wetu. Yoshua akawaambia watu, Hamwezi kumtumikia Bwana; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye
ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu. Kama mkimwacha Bwana na kuitumikia
miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema. Lakini
hao watu wakamwambia Yoshua, La! Lakini tuatamtumikia Bwana. Yoshua akawaambia watu, Ninyi mmekuwa
mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua Bwana, ili kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi.
Akasema, Basi sas, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa Bwana, Mungu wa
Israeli. Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, Bwana, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia; na sauti yake
ndiyo tutakayoitii. Basi Yoshua akafanya agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko
Shekemu. Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa,
akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa Bwana. Yoshua akawaambia
watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya Bwana
aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu. Basi Yoshua akawaruhusu watu,
wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake. Ikawa, baada ya hayo, Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa
Bwana, akafa, mwenye umri wa miaka mia na kumi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.16:1-2,5,7-8,11 (K)5
1. Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Sina wema ila utokao kwako.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.
2. Bwana ndiye fungu la posho langu,
Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku. (K)
3. Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume
Mna mema ya milele. (K)
SHANGILIO: Yak.1:18
Aleluya, aleluya!
Kwa kupenda kwake mwenyewe,
Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli,
tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya!
INJILI: Mt.19:13-15
Yesu aliletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake
wakawakemea. Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa
maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu yao, akatoka
huko.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa imani tumechagua kumtumikia Bwana
aliyetukomboa kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo, aliyezaliwa
na Bikira Maria. Kwa vile tunahitaji msaada wa Mungu, tuombe:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Maaskofu wetu na wote wenye Daraja Takatifu watekeleze
kwa vitendo ahadi na viapo vyao walivyoviweka mbele
ya Kanisa. Ee Bwana.
2. Uijalie serikali yetu kusimamia vema miongozo na
itikadi za dini mbalimbali; tupate kuishi kwa upendo
na kukuabudu kwa amani na utulivu. Ee Bwana.
3. Kila mkristo akutumikie kwa moyo mnyofu, kwa
imani safi aliyoikiri siku ya Ubatizo, yaani kukusadiki
Wewe Mungu na kumkataa shetani. Ee Bwana.
4. Uwafariji wote wenye kudhulumiwa na kuonewa
sababu ya unyonge wao; na uwaimarishe katika
imani ya kwamba kila mtu atalipwa kadiri ya
matendo yake mwenyewe. Ee Bwana.
5. Kwa maombezi ya Bikira Maria, marehemu wetu
wapewe uzima wa milele mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tukujie kwa unyenyekevu kama
watoto wadogo, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.