JUMAMOSI JUMA 18 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Kum.6:4-13
Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu. Bwana ndiye mmoja. Nawe inpende Bwana, Mungu wako. kwa moyo wako wote, na kwa roho yako vote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani. na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako. Tena itakuwa atakapokwisha Bwana, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; ndipo ujitunze, usije ukamsahau Bwana alivekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.18:1-2,46,50 (K)1
1. Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana; Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu.

(K) Wewe Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana.

2. Bwana ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu. (K)

3. Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na mzao wake hata milele. (K)

SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana,
yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,
bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!

INJILI: Mt.17:14–20
Mtu mmoja alimjia Yesu, akampigia magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nayi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa Imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na Imani kiasi cha punji ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowekana kwenu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa vile sisi tumekombolewa na Mungu kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo, tumwombe Mungu kupitia Bikira Maria tukisema:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wetu wa Kanisa waongezewe ari ya kuifundisha kwa vitendo Amri yako Kuu ya Mapendo. Ee Bwana.

2. Watawala wa dunia wakumbushwe kuvitumia daima vitu vya dunia hii kadiri ya matakwa yako, kwani vyote vimetoka kwako. Ee Bwana.

3. Utujalie sisi sote imani thabiti, tupate kukutumikia na kukutegemea Wewe; na hivi kuwaimarisha pia wenzetu katika taabu na raha. Ee Bwana.

4. Uwasikilize wanaokulilia; uwaepushe na mtu wa hila na majivuno, ili mwenye haki aishi kwa imani yake. Ee Bwana.

5. Kwa maombezi ya Bikira Maria, wagonjwa wetu wapone; na wafu wafufuliwe na kufikishwa mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu ambaye kwako yote yawezekana, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo. Bwana wetu. Amina.