JUMAMOSI JUMA 15 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.12:37-42
Wana wa Israeli walisafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi, walipata hesabu yao kama watu sita mia
elfu watu waume waliokwenda kwa miguu, bila kuhesabu watoto. Na kundi kubwa la watu waliochangamana
mno wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng'ombe, wanyama wengi sana. Nao wakaoka mikate isiyochachwa
ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri,
wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula. Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana,
muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini. Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia
nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya Bwana yalitoka nchi ya Misri. Ni
usiku wa kuangaliwa sana mbele za Bwana kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa
Bwana, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.136:1,10-15,23-24 (K)1
1. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akawatoa Waisraeli katikati yao;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
(K) Fadhili zake ni za milele.
2. Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akawavusha Israeli katikati yake;
Kwa maana fadhili zake ni za milele. (K)
3. Aliyetukumbuka katika unyonge wetu;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akatuokoa na watesi wetu;
Kwa maana fadhili zake ni za milele. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Thoma akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda,
tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?”
Aleluya!
INJILI: Mt.12:14-21
Mafarisayo walitoka wakafanya shauri juu ya Yesu jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu
hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili
litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; mpendwa wangu,
moyo wangu uliyependezwa naye; nitatia roho yangu juu yake, naye atawatangazia Mataifa hukumu.
Hatateta wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja,
wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Yesu Kristo ndiye “Mtumishi wa Bwana" ambaye, kadiri ya
nabii Isaya, moyo wa Mungu umependezwa naye. Kwa maombezi
ya Bikira Maria mamae, tumwombe tukisema:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Maaskofu na Mapadre uliowateua kuwa watumishi na watangazaji
wa Injili, waimarishwe katika kuutekeleza
wajibu huo mkubwa duniani kote. Ee Bwana.
2. Uwaponye wagonjwa na kuwasaidia wote wanaokufuata
kwa moyo mnyofu, wakiwa na matatizo mbalimbali ya kimwili
na kiroho. Ee Bwana.
3. Utusaidie sisi sote kushika kiaminifu amri zako,
kwani ni dira inayotuongoza uliko Wewe. Ee Bwana.
4. Uwaonye wote wanaotumia vibaya mamlaka yao
dhidi ya wanyonge; na uwanyenyekeshe wote
wenye kukukana na kukudharau Wewe. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe kwenye kundi la
watakatifu wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Kristo Yesu uliyesema mataifa watalitumainia jina
lako, uyapokee maombi yetu. Unayeishi na kutawala
daima na milele. Amina.