JUMAMOSI JUMA 14 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.49:29-33;50:15-25
Yakobo aliwaamuru wanawe: Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba
zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti; katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela,
iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti,
pawe milki yake pa kuzikia. Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka
mkewe; nami humo nikamzika Lea; shamba na pango iliyomo lililonunuliwa kwa bani Hethi. Basi Yakobo
alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake.
Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; nave
atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla
ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Nakuomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao,
maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu
akalia waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa
wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya,
bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Basi sasa msiogope;
mimi nitawalisha, na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema. Akakaa Yusufu katika Misri, yeye
na nyumba ya babaye. Akaishi lusuru miaka mia na kumi. Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha
tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu. Yusufu akawaambia nduguze,
Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha kutoka nchi hii, mpaka nchi
aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akisema, Bila shaka
Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:1-4,6-7 (K)Zab.69:32
1. Aleluya.
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,
Wajulisheni watu matendo yake,
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
2. Jisifuni kwa jina lake lakatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake siku zote. (K)
3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo wateule wake.
Yeye Bwana, ndiye Mungu wetu,
duniani mwote mna hukumu zake. (K)
SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
Neno la Bwana hudumu hata milele,
na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya!
INJILI: Mt.10:24–33
Yesu aliwafundisha mitume wake: Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake.
Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye
nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake? Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno
lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi
katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao
mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika
jehanum. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba
yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora ninyi kuliko
mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye
mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tunao wajibu mkubwa kwa Mungu na kwa jirani
zetu huku imani yetu ikiwa katika upinzani. Tumwombe
Mungu kupitia Mama yetu Bikira Maria tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu
na viongozi wote wa Kanisa waongezewe ujasiri katika kufundisha
imani sahihi, kuilinda na kuitetea bila woga wowote. Ee Bwana.
2. Uwajalie viongozi wa dunia kukumbuka daima, kwamba wanawaongoza
watu kwa dhamana yako Wewe, uliye Bwana wa majeshi na Mungu
Mtakatifu. Ee Bwana.
3. Waongoe ndugu zetu wanaomkana Mwanao Yesu Kristo, ili naye
asije kuwakana mbele yako huko mbinguni. Ee Bwana.
4. Uamshe ndani ya kila mmoja wetu tabia ya uwazi na ukweli; na
hivi kuondoa hofu, masengenyo na hali ya kudhaniana vibaya. Ee Bwana.
5. Kwa rehema yako, uwapokee kwako mbinguni ndugu zetu marehemu. Ee Bwana.
Ee Mungu Baba, Mwanao alisema: “Si ninyi msemao bali ni Roho wa
Baba yenu asemaye ndani yenu.” Uipokee sala yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.