JUMAMOSI JUMA 13 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.27:1-5,15-29
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia,
Mwanangu. Nave akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya
kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie
mawindo; ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki,
kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda nyikani awinde
mawindo, ayalete. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani,
akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo
yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu na mkate alioufanya. Akaja kwa
baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu? Yakobo akamwambia babaye,
Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondo- ka, tafadhali, ukae kitako,
ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna
hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu Bwana, Mungu wako, amenifanikisha. Isaka akamwambia Yakobo, Karibu,
tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo. Basi Yakobo
akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni
mikono ya Esau. Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake,
yenye malaika; basi akambariki. Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi. Akasema,
Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogeza karibu,
naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa. Isaka, baba yak, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu,
mwanangu. Akamkaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama,
harufu ya mwanangu Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana. Mungu na akupe ya umande wa mbingu,
Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo, Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie,
Uwe bwana wa ndugu zako, na wana wa mama yako na wakusujudie, atakayekulaani alaaniwe, Na
atakayekubariki abarikiwe.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.135:1-6 (K)3
1. Aleluya.
Lisifuni jina la Bwana,
Enyi watumishi wa Bwana, sifuni.
Ninyi msimamao nyumbani mwa Bwana,
Nyuani mwa nyumba ya Mungu wetu.
(K) Msifuni Bwana kwa kuwa ni mwema.
2. Msifuni Bwana kwa kuwa Bwana ni mwema.
Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza.
Kwa sababu Bwana amejichagulia Yakobo,
Na Israeli, wawe watu wake hasa. (K)
3. Maana najua ya kuwa Bwana ni mkuu.
Na Bwana wetu yu juu ya miungu yote.
Bwana amefanya kila lililompendeza,
Katika mbingu na katika nchi,
Katika bahari na katika vilindi vyote. (K)
SHANGILIO: Mt.4:4
Aleluya, aleluya!
Mtu hataishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno litokalo katika
kinywa cha Mungu.
Aleluya!
INJILI: Mt.9:14-17
Wanafunzi wake Yohane walimwendea Yesu wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali
wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana
arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.
Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande
cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu;
na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai
mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, njia za Mungu ni za ajabu na mipango yake
haitabiriki. Kwa vile kwake yote yawezekana, kwa
maombezi ya Bikira Maria, tuombe neema yake.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uzidi kulijalia Kanisa lako viongozi halali na wenye
sifa zinazokubalika mbele yako. Ee Bwana.
2. Uwajalie wazazi na viongozi wote wa jumuiya zetu
neema ya kutawala vionjo vyao; wawe na upendo
wa kweli, na siyo ubaguzi, ili haki, amani na usawa
vitawale familia na jumuiya zetu. Ee Bwana.
3. Kila mmoja wetu ajaliwe kutafuta riziki na nafasi yake
katika jamii, kwa njia halali, na hivi kutimiza
mapenzi yako. Ee Bwana.
4. Uwasamehe wadhambi, uwafariji wafungwa na
kuwaacha huru watumwa, wapate kuishi kwa amani
na raha. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wafunguliwe vifungo vyao na kushirikishwa
karamu ya arusi isiyo na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Bwana Mungu, twatamani kufika kwako ambako
hakuna maombolezo wala mfungo. Utujalie hayo yote.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.