JUMAMOSI JUMA 12 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.18:1-15
Bwana alimtokea lbrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana
wakati wa hari, Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Nave
alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana
wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe
basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo,
mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama
ulivyosema. Basi lbrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga
safi, uukande, ufanye mikate. lbrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye
laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa,
akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara
mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati uu huu mwakani, na tazama, Sara
mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi lbrahimu
na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa
hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? Bwana
akamwambia lbrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno
gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati uu huu mwakani, na Sara
atapata mwana wa kiume. Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo,
umecheka.
WIMBO WA KATIKATI: Lk.1:46-50,53-55 (K)54
1. Moyo wangu wamwadhimisha Bwana.
Na roho yangu imemfurahia
Mungu Mwokozi wangu.
(K) Bwana alikumbuka rehema zake.
2. Unyonge wa mjakazi wake.
Kwa maana, tazama, tokea sasa
Vizazi vyote wataniita mbarikiwa. (K)
3. Kwa kuwa mwenye nguvu amenitendea makuu,
Na jina lake ni takatifu.
Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi,
Kwa hao wanaomcha. (K)
4. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake:
Ili kukumbuka rehema zake.
Kama alivyowaambia baba zetu,
Ibrahimu na uzao wake hata milele. (K)
SHANGILIO: Lk.8:15
Aleluya, aleluya!
Wanabarikiwa wale walisikio
neno la Bwana na kulishika
Aleluya!
INJILI: Mt.8:5–17
Yesu alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, amsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala
nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu,
akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu, lakini sema neno tu, na mtumishi
wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu;
nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu
aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa
namna hii, kwa yeyote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki,
na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali
wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu
akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile
ile. Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwewe Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani
hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni,
wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili
litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na kuyachukua
magonjwa yetu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, umetufunulia kuwa Wewe upo pia katika nafsi
za wenzetu, hasa wale wanaohitaji msaada wetu. Kwa
vile si rahisi kuwabaini wenye nia mbaya, twakuomba:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Uwajalie viongozi wetu wa Kanisa imani thabiti,
wapate kuwaokoa waamini wao dhidi ya yule
mwovu, kwa neno lako na kwa kuadhimisha
Sakramenti zako. Ee Bwana.
2. Uwajalie wote wenye mamlaka kukuogopa Wewe
Mungu, na kuwahudumia walio chini yao kwa utu
wema, na hivi kuheshimu uhuru wao na haki za
kibinadamu. Ee Bwana.
3. Utuepushe na hila za yule mwovu katika harakati zetu
za kutimiza amri ya kukupenda Wewe na jirani. Ee Bwana.
4. Wote wenye shida wasichoke kukukimbilia Wewe
kwa sala; na uwajalie mahitaji yao yote. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu wagonjwa waponywe kwa jina lako; na
marehemu wote watakaswe dhambi zao na kuvikwa
utukufu wa ufufuko huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba Mama yetu Bikira Maria azisindikize sala
zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.