JUMAMOSI JUMA 11 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Kor.12:1-10
Sina budi kujisifu, ijapokuwa haipendezi; lakini nitafikilia maono na mafunuo ya Bwana. Namjua
mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui;
kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu.
Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui;
Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu
mwanadamu ayanene. Kwa habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu
sitajisifu, isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu. Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa
mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo
kwangu au kuyasikia kwangu. Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo
nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa
ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu
yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa
furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli,
na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:7-12
1. Malaika wa Bwana hufanya kituo,
Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.
2. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake,
Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
Wana-simba hutindikiwa, huona njaa;
Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema. (K)
3. Njoni, enyi wana, mnisikilize,
Nami nitawafundisha kumcha Bwana.
Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima,
Apendaye siku nyingi apate kuona mema? (K)
SHANGILIO: Zab.119:34
Aleluya, aleluya!
Unifahamishe nipate kuishika sheria yako,
niifuate kwa moyo wangu wote.
Aleluya!
INJILI: Mt.6:24-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili, kwa maana atamchukia
huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na
mali. Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili
yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa
angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni
huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza
kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi
yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari
yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni,
yaliyopo leo, na kesho hutupwa karibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba?
Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa
huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni
kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa
kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, maisha ni zaidi ya chakula; na mwili ni zaidi
ya mavazi. Kwa kuwa tunahitaji msaada wa Mungu,
kwa maombezi ya Bikira Maria, tuombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie viongozi wa Kanisa kujishughulisha zaidi
na kazi za kichungaji, na hivi kuwa mfano bora katika
kukutumikia Wewe. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wajaliwe kukumbuka daima, kuwa
raia wao wanahitaji na wanastahili kutengewa muda
na mahali, kwa ajili ya kukuabudu Wewe. Ee Bwana.
3. Uwakumbushe wote waliokuacha Wewe, kuwa
kutozishika amri zako ni kujitenga nawe na
kujitakia hukumu. Ee Bwana.
4. Kwa kuwa sisi sote tu dhaifu, tujaliwe nguvu ya
kushinda vishawishi na kukutegemea Wewe daima.
Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu na wote walioaga dunia wajaliwe
sasa kuuona uso wako mtukufu. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyemfanya Bikira Maria awe mwombezi
wetu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.