IJUMAA OKTAVA YA PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.4:1-12
Petro na Yohane walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo
wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo
wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini
wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano.
Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi Kuhani Mkuu,
na Kayafa pia, na Yohane na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu. Walipowaweka
katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa
Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari
ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa
Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua
katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile
lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu
katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu
litupasalo sisi
WIMBO WA KATIKATI: Zab.118:1-2,4,22-27(K)22
Haleluya.
1. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Wamchao Bwana na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
(K) Jiwe walilolikataa waashi,
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Au:
Aleluya.
2. Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu.
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
Tutashangilia na kuifurahia. (K)
3. Ee Bwana, utuokoe, twakusihi;
Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi.
Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana;
Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
Bwana ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. (K)
SHANGILIO: Zab.118:24
Aleluya, aleluya,
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
tutaishangilia na kuifurahia.
Aleluya.
INJILI: Yn.21:1-14
Baada ya hayo Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye
alijidhihirisha hivi. Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya,
na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja. Simoni Petro
aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka,
wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu. Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama
ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu. Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna
kitoweo? Wakamjibu, La. Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata.
Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. Basi yule
mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia
ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Na hao
wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa
mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. Basi waliposhuka pwani, wakaona huko
moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya
samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa
samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka.
Yesu akawaambia, Njoni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza,
U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo.
Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu.
MAOMBI
Masadukayo ambao hawakuamini juu ya ufufuko wa wafu walifadhaishwa na mafundisho au mahubiri ya
mitumne juu ya ufufuko. Kwa kuwa imani thabiti katika Yesu Mfufuka ni muhimu maishani mwetu,
twamwomba Mungu tukisema:
Kiitikio: Mungu Mtukufu, pokea ombi letu.
1. Uwaongezee viongozi wa Kanisa ujasiri wa kumshuhudia Yesu Mfufuka mbele ya mataifa.
2. Watu wote wakiri kuwa hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi
kuokolewa kwalo.
3. Utujalie kuonja uwepo wa Kristo Mfufuka katika kazi zetu za kila siku na kuyafuata maongozi
yake yeye aliyetegemeo letu.
4. Mwanao Mfufuka ajioneshe pia kwa marehemu wetu wapate kumwona yeye aliye uzima na ufufuo wetu.
Ee Baba yetu Mwema, tunakiri kwamba bila Wewe kila tufanyacho ni kazi bure. Utujalie mahitaji
yetu kadiri ya mapenzi yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.