IJUMAA KUU
MASOMO
KATIKA MATESO YA BWANA
SALA Tuombe haisemwi
Ee Bwana, kumbuka rehema zako, na, kwa ulinzi wako wa milele, uwatakatifuze watumishi wako,
ambao Kristo Mwanao aliwawekea fumbo la Pasaka kwa kumwaga damu yake. Anayeishi na kutawala
milele na milele.
AU:
Ee Mungu, kwa njia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, uliangamiza mauti, urithi wa
dhambi ya kale, iliyokuwa ikitawala vizazi vyote vya binadamu. Utujalie ili, kwa kufananishwa
naye, kama tulivyoichukua sura ya mtu wa udongo kutokana na maumbile, kadhalika tuichukue sura
ya mtu wa mbinguni, kwa kutakatifuzwa na neema. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.
SEHEMU YA KWANZA: LITURUJIA YA NENO
SOMO 1: Isa.52:13-53:12
Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana.
Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote, na
umbo lake zaidi ya wanadamu), ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa
vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu. Ni nani aliyesadiki
habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo.
Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.
Alidharauliwa na kukataliwa na watu; mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye
watu humficha nyuso zao. Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko
yetu. Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa. Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu. Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu
yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea, Kila mmoja wetu
amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini
alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni,
Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.
Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayesimulia? Maana amekatiliwa
mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi
pamoja na wabaya, Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa
na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi
yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi; Na mapenzi ya Bwana
yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake
mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki, Naye atayachukua maovu yao. Kwa
hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa
sababu alimwaga nafsi yake hata kufa. Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua
dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.31:1,5,11-13a,14-16,24.(K)Lk.23:46
1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye,
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, ee Bwana, Mungu wa kweli.
(K) Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.
2. Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu,
Naam, hasa kwa jirani zangu;
Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;
Walioniona njiani walinikimbia. (K)
3. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;
Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.
Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote. (K)
4. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)
5. Umwangaze mtumishi wako
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
Iweni hodari, mpige moyo konde,
Ninyi nyote mnaomngoja Bwana. (K)
SOMO 2: Ebr4:14-16;5:7-9
Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike
sana maungamo yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu
ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawa sawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.
Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia
wakati wa mahitaji. Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea Yule, awezaye kumwokoa na kumtoa
katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa
mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha
kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.
SHANGILIO: Flp.2:8-9
Kristo alijinyenyekeza.
Akawa mtii hata mauti,
Naam, mauti ya msalaba.
Kwa hiyo tena Mungu
alimwadhimisha mno,
Akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina.
INJILI: Yn:18:1-19,42
M. = Msomaji
W. = maneno ya Watu mbalimbali
十 = maneno ya Yesu
M.
Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo yalivyoandikwa na Mtakatifu Yohane.
Yesu anakamatwa.
M.
Wakati ule Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni;
palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti,
alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi
wake. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu na
makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha. Basi Yesu, hali akijua yote
yatakayompata, akatokea, akawaambia,
十
Ni nani mnayemtafuta?
M.
Wao wakamjibu,
W.
Ni Yesu Mnazareti.
M.
Yesu akawaambia,
十
Ni mimi.
M.
Yuda naye, aliyemsaliti, alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi
nyuma, wakaanguka chini. Basi akawauliza tena,
十
Mnamtafuta nani?
M.
Wakasema,
W.
Yesu Mnazareti.
M.
Yesu akajibu,
十
Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi, basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende
zao.
M.
Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao. Basi Simoni
Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume.
Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi Yesu akamwambia Petro,
十
Rudisha upanga alani mwake; je, kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?
Yesu mbele ya Anasi na Kayafa. Petro anamkana Yesu.
M. Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu,
wakamfunga. Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa
Kuhani Mkuu mwaka ule. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba
yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu. Wakamfuata Yesu Petro na mwanafunzi mwingine.
Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika
behewa ya kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine
aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani. Basi
yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro,
W.
Wewe nawe, je, hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu?
M.
Naye akasema,
W.
Si mimi.
M.
Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa
baridi; wakawa wakikota moto, Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto. Basi Kuhani
Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake. Yesu akamjibu,
十
Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; siku zote nalifundisha katika sinagogi na katika
hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lolote. Ya nini
kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.
M.
Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema,
W.
Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?
M.
Yesu akamjibu,
十
Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?
M.
Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu. Na Simoni Petro alikuwa akisimama
huko, anakota moto. Basi wakamwambia,
W.
Wewe nawe, je, hu mwanafunzi wake mmojawapo?
M.
Naye akakana, akasema,
W.
Si mimi.
M.
Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa sikio na Petro, akasema,
W.
Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?
M.
Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.
Yesu mbele ya Pilato.
M.
Kisha wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri; lakini wao
hawakuingia ndani ya ile Praitorio, wasije wakanajisika, bali wapate kuila Pasaka. Basi
Pilato akawatokea nje, akasema,
W.
Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?
M.
Wakajibu wakamwambia,
W.
Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako.
M.
Basi Pilato akawaambia,
W.
Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!
M.
Wayahudi wakamwambia,
W.
Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.
M.
Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionesha ni mauti gani atakayokufa. Basi Pilato
akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia,
W.
Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?
M.
Yesu akamjibu,
十
Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?
M.
Pilato akajibu,
W.
Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?
M.
Yesu akajibu,
十
Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi
wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.
M.
Basi Pilato akamwambia,
W.
Wewe u mfalme basi?
M.
Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na
kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli
hunisikia sauti yangu.
M.
Pilato akamwambia,
W.
Kweli ni nini?
M.
Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia,
W.
Mimi sioni hatia yoyote kwake. Lakini kwenu kuna desturi ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati
wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?
M.
Basi wakapiga kelele tena, na kusema,
W.
Si huyu, bali Baraba.
M.
Naye yule Baraba alikuwa mnyang'anyi. Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu. Akampiga mijeledi.
Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa
wakimwendea, wakisema,
W.
Salamu! Mfalme wa Wayahudi!
M.
Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia,
W.
Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake.
M.
Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato
akawaambia,
W.
Tazama, mtu huyu!
M.
Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema,
W.
Msulibishe! Msulibishe!
M.
Pilato akawaambia,
W.
Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.
M.
Wayahudi wakamjibu,
W.
Sisi tunayo! sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa
Mungu.
M.
Basi Pilato aliposikia neno hilo akazidi kuogopa. Akingia tena ndani ya ile Praitorio,
akamwambia Yesu,
W.
Wewe umetoka wapi?
W.
Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. Basi Pilato akamwambia,
W.
Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya
kukusulibisha?
W.
Yesu akamjibu,
十
Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu, kwa hiyo yeye aliyenitia
mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.
Yesu anahukumiwa kufa.
M.
Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua: lakini Wayahudi wakapiga makelele wakasema,
W.
Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanye kuwa mfalme humfitini Kaisari.
M.
Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu,
mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya Pasaka
yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi,
W.
Tazama, Mfalme wenu!
M.
Basi wale wakapiga kelele,
W.
Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe!
M.
Pilato akawaambia,
W.
Je, nimsulibishe Mfalme wenu?
M.
Wakuu wa Makuhani wakamjibu,
W.
Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.
M.
Basi ndipo walipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.
Yesu anasulibiwa.
M.
Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa
Kiebrania, Golgotha. Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na
mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba,
imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika
Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa
Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani. Basi wakuu wa Makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato,
W.
Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.
M.
Pilato akajibu,
W.
Niliyoandika nimeyaandika.
Askari wanagawanya mavazi ya Yesu.
M.
Nao askari walipomsulibisha Yesu waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa
kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia
tangu juu. Basi wakaambiana,
W.
Tusiipasue, lakini tuipigie kura iwe ya nani.
M.
Ili litimie andiko lile linenalo: Waligawanya nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura.
Basi ndivyo walivyofanya wale askari.
Yesu na mamae.
M.
Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye
Mariamu wa Klopa na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi
aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake,
十
Mama, tazama mwanao.
M.
Kisha akamwambia yule mwanafunzi,
十
Tazama, mama yako.
M.
Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.
Yesu anakufa.
M.
Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe,
akasema,
十
Naona kiu.
M.
Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa
hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema,
十
Imekwisha.
M.
Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.
Yesu anatobolewa ubavu.
M.
Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato,
(maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe.
Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye.
Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari
mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia,
na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli, ili ninyi nanyi mpate kusadiki.
Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie: Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko
lingine lanena: Watamtazama yeye waliyemchoma.
Yesu anazikwa.
M.
Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu (lakini kwa siri, kwa
hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa.
Basi akaenda, akauondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza),
akaleta machanganyiko ya manemane na udi, yapata ratli mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu,
wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika.
Na pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo
hajatiwa bado mtu yeyote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka
Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.
MAOMBI KWA AJILI YA WATU WOTE
I. Kwa ajili ya Kanisa takatifu
Enyi ndugu wapendwa sana, tuliombee Kanisa takatifu la Mungu, ili Mungu na Bwana wetu apende
kulijalia amani, kulikusanya na kulilinda popote duniani. Pia atujalie sisi tumtukuze Mungu
Baba Mwenyezi, katika maisha ya amani na usalama.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, uliyewafumbulia mataifa yote utukufu wako katika Kristo, uilinde
kazi ya huruma yako, ili Kanisa lako, lililoenea popote duniani, liendelee kwa imani thabiti
kuliungama jina lako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
II. Kwa ajili ya Papa
Tumwombee pia Baba mtakatifu wetu J., ili Mungu na Bwana wetu,
aliyemteua katika daraja ya uaskofu, amlinde, akae mzima na salama kwa ajili ya Kanisa lake
takatifu, apate kuliongoza taifa takatifu la Mungu.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, ambaye vitu vyote huumbwa kwa uamuzi wako, uyasikilize kwa wema
maombi yetu. Umlinde kwa huruma yako huyo Mchungaji mkuu uliyemteua kwa ajili yetu, ili jamii
ya wakristo, ambao wewe mwenyewe unawatawala, chini ya huyo Mchungaji mkuu, waongezewe mastahili
ya imani yao. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
III. Kwa ajili ya kila daraja na cheo cha waamini
Tumwombee pia askofu wetu J., maaskofu wote, mapadri, mashemasi wa
Kanisa, na jamii yote ya waamini.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, ambaye Roho wako hutakatifuza na kusimamia mwili wote wa Kanisa,
utusikilize sisi tunaowaombea watumishi wako, ili wote, kwa msaada wa neema yako, wakutumikie
kiaminifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
IV. Kwa ajili ya wakatekumeni
Tuwaombee pia wakatekumeni (wetu), ili Mungu
na Bwana wetu azibue masikio ya mioyo yao na
afungue mlango wa rehema yake, kusudi, wakiisha kupata maondoleo ya dhambi zao zote kwa njia
ya maji ya Ubatizo wa kuzaliwa upya, nao pia wawemo ndani ya Yesu Kristo Bwana wetu.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, unayelisitawisha daima Kanisa lako kwa kulipatia wana wapya
Uwaongezee imani na akili wakatekumeni (wetu),
ili wakiisha kuzaliwa mara ya pili katika
kisima cha Ubatizo, wahesabiwe kati ya jamii ya hao uliowafanya watoto wako. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
V. Kwa ajili ya umoja wa Wakristo
Tuwaombee pia ndugu wote wanaomwamini Kristo, ili Mungu na Bwana wetu apende kuwakusanya
katika Kanisa lake lililo moja na kuwalinda hao, watendao ukweli.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, unayeyakusanya yaliyotawanyika na kuyalinda yaliyokusanywa,
ulitazame kwa wema kundi lake Mwanao, ili, wale waliotakaswa kwa Ubatizo mmoja, waunganishwe
kwa umoja wa imani na kifungo cha mapendo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
VI. Kwa ajili ya Wayahudi
Tuwaombee pia Wayahudi, ambao Mungu Bwana wetu alinena nao kwanza, ili awajalie wazidi kulipenda
jina lake na kuwa waaminifu katika kuishi agano lake.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, uliyempa Ibrahimu na uzao wake ahadi zako, usikilize kwa wema
maombi ya Kanisa lako, ili taifa hilo ulilojipatia kwanza lijaliwe kuufikia utimilifu wa
ukombozi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
VII. Kwa ajili ya wasiomwamini Kristo
Tuwaombee pia wale wasiomwamini Kristo, ili, wakiangazwa kwa nuru ya Roho Mtakatifu, wapate
nao kuingia katika njia ya wokovu.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, uwajalie wale wasiomwungama Kristo, na wanaenenda mbele ya uso
wako kwa moyo mnyofu, waupate ukweli. Nasi, kwa kuzidi daima katika kupendana na kwa kufanya
bidii kulifahamu kikamilifu fumbo la uzima wako, utufanye tuwe mashahidi kamili wa mapendo
yako ulimwenguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
VIII. Kwa ajili ya wasiomwamini Mungu
Tuwaombee pia wale wasiomwamini Mungu, ili, kwa kuyafuata kwa moyo mnyofu yaliyo mema,
wastahili kumfikia Mungu mwenyewe.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, umewaumba wanadamu wote, ili wakutafute daima kwa hamu na
wakikupata watulie. Tunakuomba utujalie ili, watu wote, licha ya vizuizi vyovyote vya uovu,
kwa kuzipokea ishara za wema wako na ushuhuda wa matendo mema ya wale wanaokuamini, wapate
kufurahi katika kukuungama wewe uliye peke yako Mungu wa kweli na Baba yetu sisi binadamu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
IX. Kwa ajili ya viongozi wa Serikali
Tuwaombee pia viongozi wote wa serikali, ili Mungu na Bwana wetu aelekeze akili na mioyo yao
kadiri ya mapenzi yake, kusudi watu wote wapate amani na uhuru wa kweli.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, mioyo ya watu na haki za mataifa zimo mikononi mwako. Uwaangalie
kwa wema wale wenye madaraka ya kutuongoza sisi, kusudi, kwa majaliwa yako, wadumishe popote
duniani usitawi wa mataifa, usalama wa amani na uhuru wa dini. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
X. Kwa ajili ya wenye taabu
Enyi ndugu wapendwa sana, tumwombe Mungu Baba mwenyezi, ili atakase ulimwengu na upotovu
wowote, aondoe magonjwa, afukuze njaa, ayafungue magereza, azifungue pingu. Wanaosafiri
wajaliwe usalama, walio mbali warudi makwao, wagonjwa wapone na wanaokufa waokoke.
Sala katika ukimya. Halafu kuhani anasema:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, ndiwe faraja ya wenye kusikitika, na nguvu ya wanaoteswa. Yafike
kwako maombi ya wanaokulilia katika taabu yoyote, ili, kwa rehema yako, wote, kila mmoja katika
shida yake, wafurahie kusikilizwa. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, umetuhuisha kwa njia ya kifo kitakatifu na ufufuko wa Kristo wako.
Tunakuomba, udumishe ndani yetu kazi ya rehema yako, ili, kwa kushiriki fumbo hili takatifu,
tupate kuishi katika uchaji siku zote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
SALA JUU YA WATU:
Ee Bwana, tunakuomba, baraka zako nyingi ziwashukie watu wako, ambao wamekumbuka kifo cha
Mwanao kwa kutazamia kufufuka kwao; wapate rehema, wajaliwe kitulizo, waongezewe imani takatifu,
na wathibitishiwe ukombozi wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.