Generic placeholder image

IJUMAA BAADA YA KUPAA BWANA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.

Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.

Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.

Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.

Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.

Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.

Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.


2 (33) Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.

E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!

Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.

Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.

Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.

Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.

Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.

3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;

Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;

Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.

Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal

4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.

Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.

Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.

Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434

5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.

Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.

Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930

ANT. I: Bwana ameniokoa kutoka katika nguvu za mauti, aleluya.

Zab.116:1-9 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika Ufalme wa Mungu(Mate.14:22)

Nampenda Mungu, kwa maana anisikia,*
maana amesikiliza kilio cha ombi langu.

Yeye hunisikiliza*
kila ninapomlilia.

Hatari ya kifo ilinizunguka,/
vitisho vya kaburi vilinivamia;*
nilijawa mahangaiko na majonzi.

Kisha nikamlilia Mungu:*
"Ee Mungu, tafadhali unisalimishe!”

Mungu amejaa wema na haki;*
Mungu wetu ni mwenye huruma.

Mungu huwalinda wanyofu;*
nilikuwa nimekandamizwa, naye akaniokoa.

Uwe na utulivu mkuu, ee roho yangu,*
kwa maana Mungu amenitendea vyema.

Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;*
akanilinda nisije nikaanguka.

Basi, nitatembea mbele yake Mungu,*
katika nchi ya watu walio hai.

Asifiwe Mungu, Mungu wa Israeli!*
Asifiwe sasa na milele!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana ameniokoa kutoka katika nguvu za mauti, aleluya.

ANT. II: Bwana aliwalinda watu wake, kama mboni ya jicho lake, aleluya.

Zab.121 Mungu kinga yetu
Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena(Ufu.7:16)

Ninatazama huko juu milimani;*
msaada wangu watoka wapi?

Msaada wangu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.

Hatakuacha uanguke;*
mlinzi wako hasinzii.

Mlinzi wa Israeli*
hasinzii wala halali.

Mungu anakulinda na kukukinga;*
yuko pamoja nawe kukulinda.

Mchana jua halitakuumiza,*
wala mwezi wakati wa usiku.

Mungu anakukinga na majanga yote;*
anayalinda salama maisha yako.

Anakulinda ujapo na uendapo,*
sasa na hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana aliwalinda watu wake, kama mboni ya jicho lake, aleluya.

ANT. III: Bwana ni nguvu na kinga yangu, yeye ni wokovu wangu, aleluya.

WIMBO: Ufu.15:3-4 Utenzi Wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!

Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!

Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.

Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana ni nguvu na kinga yangu, yeye ni wokovu wangu, aleluya.

SOMO: Ebr.5:8-10
Ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kwa njia ya mateso kutii. Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii, naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.

KIITIKIZANO
K. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Atawafundisheni kila kitu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Roho...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao, aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Kristo, aliyeshukiwa na Roho Mtakatifu.
W. Kristo uliyetukuzwa, utuombee.

Bwana Yesu, uwaangalie Wakristo pote ulimwenguni;
- uwakusanye katika umoja kwa njia ya Roho wako Mtakatifu. (W.)

Uwape mwanga wako wale wote wanaodhulumiwa kwa ajili ya jina lako;
- uwajalie waweze kujua nini cha kuwaambia watesi wao. (W.)

Uwawezeshe watu wote wakujue wewe, uliye pekee mzabibu wa kweli;
- uwafanye wawe matawi yako yenye kuzaa matunda ya Roho. (W.)

Mfalme wa ulimwengu, ulipaa mbinguni, ukawafurahisha malaika na watu;
- uumiliki ulimwengu wetu, na uyatawale mataifa yote. (W.)

Umewashirikisha waliobatizwa kifo na ufufuko wako;
- saa ya kufa kwao uingie nao katika uzima wa milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, watupatia uzima wa milele kwa ufufuko wa Mwokozi wetu, ambaye anatawala nawe akiwa ameketi mkono wako wa kuume; utuweke nasi kuumeni kwako. Ulituzaa upya katika ubatizo: Kristo atakapokuja katika utukufu wake, utuvishe vazi la furaha ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.