IJUMAA BAADA YA KUPAA BWANA
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo Bwana ametuahidi Roho Mtakatifu: njooni, tumwabudu, aleluya.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.
Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.
Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.
Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.
Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.
Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.
Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.
2 (33)
Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.
E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!
Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.
Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.
Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.
Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.
Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.
3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;
Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;
Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.
Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal
4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.
Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.
Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.
Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434
5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.
Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.
Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930
ANT. I: Jipe moyo, mwanangu, umesamehewa dhambi zako, aleluya.
Zab.51 Kuomba msamaha
Jirekebisheni upya rohoni na katika fikra zenu. Vaeni hali mpya ya utu (Ef.4:23-24)
Unihurumie, Ee Mungu,*
kwa sababu ya upendo wako mkuu;
ufutilie mbali uovu wangu,*
kwa sababu ya huruma yako kuu.
Unioshe kabisa kosa langu;*
unisafishe dhambi yangu.
Nakiri kabisa makosa yangu,*
daima naiona waziwazi dhambi yangu.
Nimekukosea wewe peke yako,*
nimetenda yaliyo mabaya mbele yako.
Hivyo wafanya sawa unaponihukumu,*
una haki kabisa unaponiadhibu.
Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu,*
mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu.
Wewe wataka unyofu wa ndani;*
hivyo nifundishe hekima moyoni.
Uniondolee dhambi, nitakate;*
unioshe, niwe mweupe pе.
Hapo nitaweza kufurahi tena;*
nitashangilia tena ingawa uliniponda.
Ugeuze uso wako, usiziangalie dhambi zangu;*
ukayafute makosa yangu yote.
Ee Mungu, uniumbie moyo safi,*
uweke ndani yangu roho mpya na thabiti.
Usinitupe mbali nawe;*
usiniondolee Roho wako mtakatifu.
Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa,*
unijalie moyo radhi wa utii.
Hapo nitawafundisha wakosefu mwongozo wako,*
nao wenye dhambi watarudi kwako.
Ee Mungu, Mungu mwokozi wangu, uniokoe na kifo,*
nami nitatangaza kwa furaha uadilifu wako.
Ifumbue midomo yangu, Ee Bwana,*
nipate kutangaza sifa zako.
Kwa kweli wewe hupendezwi na sadaka,/
ama sivyo mimi ningalikutolea.*
Wewe huna haja na sadaka za kuteketezwa.
Sadaka yangu kwako, Ee Mungu, ni moyo mnyofu;*
wewe, Ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu.
Ee Mungu, uutendee mji Sion mema:*
jenga tena upya kuta za Yerusalemu.
Hapo utapendezwa na sadaka za kweli;/
dhabihu na sadaka za kuteketezwa*
na fahali watatolewa sadaka madhabahuni pako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Jipe moyo, mwanangu, umesamehewa dhambi zako, aleluya.
ANT. II: Bwana, ulikuja na nguvu kuwaokoa watu wako; ulikuja na
Kristo wako, aleluya.
WIMBO: Hab.3:2-4,13a,15-19
Simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia (Lk.21:28)
Ee BWANA, nimesikia habari zako,*
Nami naogopa;
Ee BWANA, fufua kazi yako katikati ya miaka;/
Katikati ya miaka tangaza habari yake; *
Katika ghadhabu kumbuka rehema.
Mungu alikuja kutoka Temani,*
Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani.
Utukufu wake ukazifunika mbingu,*
Nayo dunia ikajaa sifa yake.
Mwangaza wake ulikuwa kama nuru;/
Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake;*
Ndipo ulipofichwa uweza wake.
Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako,*
Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako;.
Ukaikanyaga bahari kwa farasi zako,*
Chungu ya maji yenye nguvu.
Nikasikia, na tumbo langu likatetemeka,*
Midomo yangu ikatikisika kwa sauti ile;
Ubovu ukaingia mifupani mwangu,*
Nikatetemeka katika mahali pangu;
Ili nipate kuingoja ile siku ya dhiki,*
Kundi lao washambuliao wakweapo juu ya watu.
Maana mtini hautachanua maua,*
Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda;
Taabu ya mzeituni itakuwa bure,*
Na mashamba hayatatoa chakula;
Zizini hamtakuwa na kundi,*
Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe.
Walakini nitamfurahia BWANA,*
Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.
BWANA ni nguvu zangu,/
Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu,*
Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Bwana, ulikuja na nguvu kuwaokoa watu wako; ulikuja na
Kristo wako, aleluya.
ANT. III: Sion, msifu Mungu wako, kwani ameleta amani katika nchi
yako, aleluya.
Zab.147:12-20 Ni vizuri kumsifu Mungu
Njoo! Mimi nitakuonesha bibi arusi, mkewe Mwana-kondoo! (Ufu.21:9)
Ee Yerusalemu, umsifu Mungu!*
Umsifu Mungu wako, ee Sion!
Maana ameiimarisha milango yako,*
amewabariki watu waliomo kwako.
Ameweka amani mipakani mwako;*
anakushibisha kwa ngano safi kabisa.
Yeye hupeleka amri yake duniani,*
na neno lake hutekelezwa upesi.
Hutandaza theluji kama pamba,*
hutawanya umande kama majivu.
Huleta mvua ya mawe/
vipande vikubwa vikubwa kama mkate*
na kwa ubaridi wake maji huganda.
Kisha hutoa amri, na maji hayo huyeyuka;*
huvumisha upepo wake, nayo hutiririka.
Humjulisha Yakobo ujumbe wake,*
na Israeli amri na maagizo yake.
Lakini watu wengine hakuwafanyia hayo;*
watu wengine hawayajui maagizo yake.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Sion, msifu Mungu wako, kwani ameleta amani katika nchi
yako, aleluya.
SOMO: Mate.5:30-32
Mungu wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya ninyi kumwua kwa kumtundika msalabani. Huyu ndiye
yule aliyekwezwa na Mungu mpaka upande wake wa kulia, akawa Kiongozi na Mkombozi, ili awawezeshe
watu wa Israeli kutubu, wapate kusamehewa dhambi zao. Sisi ni mashahidi wa tukio hilo, naye Roho
Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii, anashuhudia pia tukio hilo.
KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Katika Yesu tunamwona yeye ambaye amevikwa sasa taji ya utukufu na heshima, kwa sababu aliuawa,
aleluya.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Katika Yesu tunamwona yeye ambaye amevikwa sasa taji ya utukufu
na heshima, kwa sababu aliuawa, aleluya.
MAOMBI
Tumwombe Kristo, aliyepaa mbinguni ili awapelekee mitume Roho Mtakatifu.
W. Umtume Roho wako kwetu.
Bwana, utushushie Roho Mtakatifu tuliyeahidiwa na Baba;
- utushushie nguvu kutoka juu. (W.)
Ulitaka wanafunzi wako wawe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa:
- kwa Roho wako, utufundishe hekima na unyofu. (W.)
Sasa umeketi mkono wa kuume wa Baba;
- utuombee sasa, tunapokutazamia kwa matumaini, wewe uliye Kuhani wetu wa Milele. (W.)
Utuwezeshe kushiriki mateso yako tunapopatwa na huzuni;
- utujalie tufufuke pamoja nawe katika utukufu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tunapoungojea ujio wa utawala wa Mungu, tusali tukisema:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, watupatia uzima wa milele kwa ufufuko wa Mwokozi wetu, ambaye anatawala nawe akiwa
ameketi mkono wako wa kuume; utuweke nasi kuumeni kwako. Ulituzaa upya katika ubatizo: Kristo
atakapokuja katika utukufu wake, utuvishe vazi la furaha ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya
Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na
milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.