IJUMAA JUMA LA 7 PASAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa.
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpya.
Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga,
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.
Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
Zab.22 Kilio (Zaburi ya Daudi)
Yesu akalia kwa sauti kubwa:"Eli, Eli, lama sabakthani?” (Mt.27:46)
I
Mungu wangu, Mungu wangu!*
Kwa nini umeniacha?
Mbona uko mbali sana kunisaidia,*
mbali na maneno ya kilio changu?
Mungu wangu! Nalia mchana lakini husikilizi;*
napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati.
Hata hivyo, wewe ni mtakatifu;*
wewe unayesifiwa na watu wa Israeli.
Wazee wetu walikutegemea;*
walikutegemea, nawe ukawaokoa.
Walikulilia hatarini, wakasalimika;*
walikutumainia, nao hawakuaibika.
Lakini mimi ni mdudu tu, wala si mtu;*
nimepuuzwa na kudharauliwa na kila mtu.
Wote wanionao wananicheka;*
wananifyonya na kutikisa vichwa.
Wanasema: "Si ulimtumainia Mungu?*
Kwa nini sasa hakuokoi?
Kama anapendezwa nawe,*
basi, na akusalimishe!"
Lakini wewe, Ee Mungu,/
ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,*
na kunilinda nilipokuwa mtoto mchanga.
Nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu;*
tangu nilipozaliwa wewe u Mungu wangu.
Usikae mbali nami, kwani taabu imekaribia;*
uwe karibu, maana hakuna wa kunisaidia.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Adui wengi wanizunguka kama fahali;*
wamenisonga kama fahali wakali wa Bashani!
Wanafunua vinywa vyao kama simba,*
tayari kunishambulia na kunirarua.
Nimekwisha kama maji yaliyomwagika;/.
mifupa yangu yote imeteguka;*
moyo wangu ni kama nta iliyoyeyuka.
Koo langu limekauka kama kigae;/
ulimi wangu wanata kinywani mwangu.*
Umeniacha mfu mavumbini.
Genge la waovu limenizunguka;/
wananizingira kama kundi la mbwa;*
mikono na miguu wamenitoboa.
Nimebaki mifupa mitupu;*
adui zangu waniangalia na kunisimanga.
Wanagawiana nguo zangu;*
wanalipigia kura vazi langu.
Ee Mungu, usisimame mbali nami.*
Ewe unisaidiaye, uje upesi kunisaidia.
Niokoe na upanga!*
Niepushe na mbwa hawa!
Niokoe kinywani mwa simba;*
mimi ni dhaifu mbele ya nyati hawa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
III Shukrani
Nitawatangazia ndugu zangu matendo yako;*
nitakusifu katika jamii yao:
"Enyi watumishi wa Mungu, msifuni!/
Enyi wana wa Yakobo, mtukuzeni Mungu;*
enyi watu wote wa Israeli, mwabuduni.
Maana yeye hadharau unyonge wa maskini,/
wala kupuuza mateso yao;*
hawapi kisogo, bali huwajibu wamwombapo msaada."
Wewe wanijalia kukusifu/
katika jamii kubwa ya watu;*
nitatimiza nadhiri zangu mbele yao wakuchao.
Maskini watakula na kushiba;/
wanaomtafuta Mungu watamsifu.*
Wafanikiwe milele!
Ulimwengu wote utakumbuka/
na kumrudia Mungu;*
jamaa zote za mataifa zitamwabudu.
Maana Mungu ni mfalme;*
yeye anayetawala mataifa.
Wenye kiburi wote watasujudu mbele yake;*
wote ambao hufa watamwabudu.
Vizazi vijavyo vitamtumikia;*
watu watavisimulia habari za Bwana,
na watatangaza matendo yake ya wokovu,/
kwa watu wasiozaliwa bado;*
kwamba: “Mungu amefanya hayo!”
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Mate.2:32,36
Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu, na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. Ni lazima watu
wote wa Israeli wafahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulibisha ninyi, ndiye huyo ambaye
Mungu amemfanya kuwa Bwana na Masiha.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Gal.3:27-28
Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena
tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu
kimoja katika kuungana na Kristo Yesu.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: 1Kor.5:7,8
Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama
mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa sadaka. Basi, tufanye karamu
hiyo sio kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu,
mkate wa usafi na ukweli.
K. Kaa nasi,Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.
SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ulitufungulia njia ya kuufikia uzima wa milele Kristo Mwanao alipopalizwa
juu na kutukuzwa, na Roho wako Mtakatifu alipofika kuliangazia Kanisa lako. Utujalie, tunaposhiriki
zawadi kubwa namna hii, imani yetu iimarike zaidi na zaidi, na ibada yetu iwe ya uchaji zaidi na
zaidi. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.