Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 7 PASAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.

Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.

Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.

Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.

Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.

Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.

Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.


2 (33) Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.

E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!

Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.

Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.

Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.

Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.

Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.

3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;

Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;

Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.

Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal

4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.

Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.

Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.

Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434

5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.

Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.

Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930

ANT. I: Mimi, niliye Bwana, ni Mwokozi wako; mimi ni Mkombozi wako, aleluya.

Zab.135 Sifa kwa Mungu
Ninyi ni ukoo mteule, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu (1Pet.2:9)

I
Lisifuni jina la Mungu,*
enyi watumishi wa Mungu,

mnaosimama nyumbani mwa Mungu,*
Hekaluni mwa Mungu wetu.

Msifuni Mungu kwa kuwa ni mwema;*
liimbieni jina lake sifa, maana inafaa.

Mungu amejichagulia Yakobo kuwa wake,*
watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe.

Najua hakika kuwa Mungu ni mkuu;*
Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote.

Mungu hufanya yote anayotaka,*
mbinguni, duniani, baharini na vilindini.

Huleta mawingu kutoka mipaka ya dunia;/
hufanya gharika kuu kwa umeme,*
na huvumisha upepo kutoka ghala zake.

Aliwaua wazaliwa wa kwanza kule Misri,*
wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika.

Alifanya ishara na maajabu kwako, Ee Misri,*
dhidi ya Farao na maofisa wake wote.

Aliyaangamiza mataifa mengi,*
akawaua wafalme wenye nguvu:

akina Sihoni, mfalme wa Waamori,*
na Ogu, mfalme wa Bashani, na wafalme wote wa Kanaani.

Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake;*
aliwapa Waisraeli ziwe urithi wao.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Mimi, niliye Bwana, ni Mwokozi wako; mimi ni Mkombozi wako, aleluya.

ANT. II: Umebarikiwa ufalme wa Daudi baba yetu, ambao umetujia, aleluya.

II
Ee Mungu, jina lako lakumbukwa milele,*
utakumbukwa na watu wa vizazi vyote.

Maana Mungu atawatetea watu wake;*
atakuwa na huruma kwa watumishi wake.

Miungu ya mataifa ni fedha na dhahabu,*
imetengenezwa na mikono ya binadamu.

Ina vinywa, lakini haisemi;*
ina macho, lakini haioni.

Ina masikio, lakini haisikii;*
wala haiwezi hata kuvuta pumzi.

Wote walioifanya wafanane nayo,*
naam, kila mmoja anayeitegemea!

Enyi watu wa Israeli, mtukuzeni Mungu!*
Enyi makuhani, wazao wa Aroni, mtukuzeni Mungu!

Enyi Walawi, mtukuzeni Mungu!*
Enyi wachaji wa Mungu, mtukuzeni.

Atukuzwe Mungu katika Sion,*
katika makao yake Yerusalemu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Umebarikiwa ufalme wa Daudi baba yetu, ambao umetujia, aleluya.

ANT. III: Tumwimbie Bwana, kwa kuwa ushindi wake ni mkuu, aleluya.

WIMBO: Ufu.15:3-4. Utenzi wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!

Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!

Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.

Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Tumwimbie Bwana, kwa kuwa ushindi wake ni mkuu, aleluya.

SOMO: Gal.5:16,22a,25
Basi, nasema hivi: mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake.

KIITIKIZANO
K. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Atawafundisheni kila kitu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Roho...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Wote, pamoja na Maria, mama yake Yesu, waliendelea kusali, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Wote, pamoja na Maria, mama yake Yesu, waliendelea kusali, aleluya.

MAOMBI
Tumtukuze Baba ambaye ameyapa mataifa neema ya Roho Mtakatifu.
W. Neema ya Roho huyo na ienee ulimwenguni.

Baba, ulitupatia Mwanao mpendwa, awe nuru kwa ajili ya mataifa;
- uyafumbue macho ya ulimwengu, ili ulimwengu uweze kumwona Kristo kuwa ndiye tarajio la wanadamu. (W.)

Ulimjaza Kristo nguvu ya Roho Mtakatifu, apate kuiendesha kazi yake ya wokovu;
- tunaomba apite tena kati yetu, akiwaponya wagonjwa na kumtendea mema kila mmoja. (W.)

Umtume Roho wako Mtakatifu, awaburudishe waliochoka, na atuimarishie imani yetu;
- uwape uzima na furaha waliovunjika moyo. (W.)

Uwatendee kadiri ya matumaini yao waamini marehemu;
- uwafufue katika utukufu Kristo atakapokuja tena. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, ulitufungulia njia ya kuufikia uzima wa milele Kristo Mwanao alipopalizwa juu na kutukuzwa, na Roho wako Mtakatifu alipofika kuliangazia Kanisa lako. Utujalie tunaposhiriki zawadi kubwa namna hii, imani yetu iimarike zaidi na zaidi, na ibada yetu iwe ya uchaji zaidi na zaidi. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.