IJUMAA JUMA LA 6 PASAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.
Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie -
Ulio mwetu mioyoni -
Mioyo mingine iwashwe.
Kutokana na mwako wake.
Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
Zab.119:73-80 X Uadilifu wa sheria ya Mungu
Wewe mwenyewe umeniumba na kunitegemeza;*
unijalie akili nijifunze maagizo yako.
Wakuchao wataniona na kufurahi,*
kwa sababu nimelitumainia neno lako.
Najua kwamba hukumu zako ni adili, Ee Mungu,*
na kwamba umeniadhibu kwani wewe ni mwaminifu.
Upendo wako mkuu wanifariji,*
kama ulivyoniahidi mimi mtumishi wako.
Unionee huruma nipate kuishi,*
maana sheria yako ni furaha yangu.
Wenye kiburi waaibike maana wamenifanyia hila,*
lakini mimi nitayatafakari maagizo yako.
Wote wakuchao na waje kwangu,*
wapate kuzijua kanuni zako.
Nizishike amri zako kikamilifu,*
nisije nikaaibishwa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.59:1-4,9-10,16-17 Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
Maneno haya ya Mwokozi na yawafundishe watu wote kumtumainia Baba yake kama
watoto wachaji (Eusebius wa Kaisaria)
Ee Mungu wangu, uniokoe na adui zangu;*
unikinge na hao wanaonishambulia.
Uniokoe na hao watu waovu;*
unisalimishe na hao wauaji!
Tazama! Wananivizia waniue;*
watu wakatili wanajiunga dhidi yangu.
Bila ya kosa, hatia au dhambi yangu,/
wanakimbia, Ee Mungu, kujiweka tayari.*
Uinuke, Ee Mungu, ukatazame na kunisaidia!
Nitakuimbia sifa, ewe uliye nguvu yangu;*
maana wewe, Ee Mungu, ni ngome yangu.
Mungu wangu atanijia kwa upendo wake mkuu,*
ataniwezesha mpaka niwaone adui zangu wameshindwa.
Lakini mimi nitaimba sifa za nguvu yako;*
nitashangilia upendo wako mkuu asubuhi;
maana wewe umekuwa ngome yangu imara,*
na kimbilio langu wakati wa shida.
Ewe uliye nguvu yangu, nitakusifu;/
Ee Mungu, wewe u ngome yangu;*
Mungu unayenipenda!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.60 Ushindi baada ya kushindwa
Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini. jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu(Yoh.16:33)
Ee Mungu, umetutupa na kututawanya*
umewaka hasira, tafadhali uturudishe.
Umeitetemesha nchi na kuipasua;*
uzibe nyufa zake kwani inabomoka.
Umewatwika watu wako mateso;*
tunayumbayumba kama waliolewa mvinyo.
Umewaashiria wale wanaokuheshimu,*
wapate kuukwepa mshale.
Uwasalimishe hao watu uwapendao;*
utuokoe kwa mkono wako, na kutusikiliza.
Mungu amesema kutoka patakatifu pake:/
"Sasa nitakwenda kwa shangwe kuigawa Shekemu;*
bonde la Sukoti nitaligawa sehemu sehemu.
Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu;/
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,*
na Yuda ni fimbo yangu ya enzi.
Moabu ni kama bakuli langu la kunawia,/
kiatu changu nitakitupia Edomu ili kuimiliki.*
Nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia.“
Ni nani atakayenipeleka kwenye mji wa ngome?*
Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?
Je, umetuacha kabisa, Ee Mungu?*
Je, huendi tena na majeshi yetu?
Utupatie msaada dhidi ya adui zetu,*
maana msaada wa binadamu haufai kitu.
Tutashinda, Mungu akiwa upande wetu,*
yeye atawaponda adui zetu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Mate.2:32,36
Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu, na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. Ni lazima watu
wote wa Israeli wafahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulibisha ninyi, ndiye huyo ambaye
Mungu amemfanya kuwa Bwana na Masiha.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Gal.3:27-28
Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena
tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu
kimoja katika kuungana na Kristo Yesu.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: 1Kor.5:7,8
Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama
mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa sadaka. Basi, tufanye karamu
hiyo sio kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu,
mkate wa usafi na ukweli.
K. Kaa nasi,Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.
SALA:
Tuombe: Bwana, isikie sala yetu. Umtume kwa watu wote Roho anayetufanya tuwe wana wako, kama
alivyobashiri Kristo, shahidi wa ukweli wako: na hivi uikamilishe, kwa njia ya injili, kazi ya
kutakatifuza, iliyoahidiwa na Neno wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.