IJUMAA JUMA LA 6 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.18:9-18
Bwana alimwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi
ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu
wengi katika mji huu. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno
la Mungu. Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja,
wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema, Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume
cha sheria. Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa
jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi; bali
ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki
kuwa mwamuzi wa mambo hayo. Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu. Nao wote wakamshika
Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo
kuwa ni kitu. Baada ya hayo Paulo akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri
kwenda Shamu; na Prisila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko
Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.47:1-6(K)7
1. Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au:
Aleluya.
2. Atawatiisha watu wa nchi chini yetu,
Na mataifa chini ya miguu yetu.
Atatuchagulia urithi wetu,
Fahari ya Yakobo ambaye alimpenda. (K)
3. Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K)
SHANGILIO: Yn.10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema,
nao walio wangu nawajua,
nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI: Yn.6:52-59
Siku ile Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza,
bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. Mwanamke
azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika, lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile
dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni. Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini
mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye. Tena siku ile
hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina
langu.
MAOMBI
Ndugu, tunapoungojea ujio wa Roho Mtakatifu, tuombe:
1. Ee Roho Mtakatifu unayeitwa muumbaji, mfariji, paji la Mwenyezi Mungu, chanzo cha uzima, moto, pendo
na mpako wa rohoni, twakuomba utujie, utazame roho zetu na utujaze neema za mbinguni.
2. Ewe mwenye kutoa vipaji saba, na kidole chake Mungu, uliyeahidiwa na Baba na mwenye kusemesha ndimi
zetu, twakuomba uje ututie nuru akilini na upendo mioyoni na, kwa imara ya kudumu, utegemeze miili yetu.
3. Uje ufukuze mashetani na kurudisha amani iliyopotea na hivi uwe kiongozi wetu tupate kuepukana na
maovu yote.
4. Umjulishe kwetu Baba, tupate kumjua pia Mwana na tukakusadiki wewe utokaye kwa Baba na Mwana.
Ee Mungu, umefundisha mioyo ya waamini kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu. Utujalie katika Roho huyo kutambua
na kupendelea mema na kufurahia daima faraja yake. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo, Bwana wetu. Amina.