IJUMAA JUMA LA 6 PASAKA
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!
Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!
Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!
Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534
2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ
3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.
Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876
4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.
Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.
Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.
Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.
Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.
Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.
Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.
Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7
5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.
Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.
Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal
6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.
Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.
Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750
7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.
Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.
Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.
Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.
Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695
ANT. I: Bwana ameniokoa kutoka katika nguvu za mauti, aleluya.
Zab.116:1-9 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika Ufalme wa Mungu(Mate.14:22)
Nampenda Mungu, kwa maana anisikia,*
maana amesikiliza kilio cha ombi langu.
Yeye hunisikiliza*
kila ninapomlilia.
Hatari ya kifo ilinizunguka,/
vitisho vya kaburi vilinivamia;*
nilijawa mahangaiko na majonzi.
Kisha nikamlilia Mungu:*
"Ee Mungu, tafadhali unisalimishe!”
Mungu amejaa wema na haki;*
Mungu wetu ni mwenye huruma.
Mungu huwalinda wanyofu;*
nilikuwa nimekandamizwa, naye akaniokoa.
Uwe na utulivu mkuu, ee roho yangu,*
kwa maana Mungu amenitendea vyema.
Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;*
akanilinda nisije nikaanguka.
Basi, nitatembea mbele yake Mungu,*
katika nchi ya watu walio hai.
Asifiwe Mungu, Mungu wa Israeli!*
Asifiwe sasa na milele!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Bwana ameniokoa kutoka katika nguvu za mauti, aleluya.
ANT. II: Bwana aliwalinda watu wake, kama mboni ya jicho lake,
aleluya.
Zab.121 Mungu kinga yetu
Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena(Ufu.7:16)
Ninatazama huko juu milimani;*
msaada wangu watoka wapi?
Msaada wangu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.
Hatakuacha uanguke;*
mlinzi wako hasinzii.
Mlinzi wa Israeli*
hasinzii wala halali.
Mungu anakulinda na kukukinga;*
yuko pamoja nawe kukulinda.
Mchana jua halitakuumiza,*
wala mwezi wakati wa usiku.
Mungu anakukinga na majanga yote;*
anayalinda salama maisha yako.
Anakulinda ujapo na uendapo,*
sasa na hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Bwana aliwalinda watu wake, kama mboni ya jicho lake,
aleluya.
ANT. III: Bwana ni nguvu na kinga yangu, yeye ni wokovu wangu,
aleluya.
WIMBO: Ufu.15:3-4 Utenzi Wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!
Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Bwana ni nguvu na kinga yangu, yeye ni wokovu wangu,
aleluya.
SOMO: Ebr.5:8-10
Ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kwa njia ya mateso kutii. Na alipofanywa mkamilifu,
akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii, naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.
KIITIKIZANO
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Walipomwona Bwana.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wanafunzi...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao, aleluya.
MAOMBI
Tumwombe Kristo, chemchemi ya uzima, na chanzo cha fadhila.
W. Bwana, anzisha tena utawala wako duniani.
Yesu, Mwokozi wetu, uliuawa na kufufuliwa;
- utujalie tuweze kuwa wafu kuhusu dhambi, na tuishi katika nguvu ya ufufuko wako. (W.)
Uliwatuma wanafunzi wako kutangaza ulimwenguni kote habari njema ya wokovu;
- wale wote wanaohubiri neno lako watiwe nguvu na Roho Mtakatifu. (W.)
Ulipewa mamlaka yote mbinguni na duniani, ili upate kuushuhudia ukweli;
- iongoze mipango ya serikali na watawala, ifuate ukweli.
(W.)
Uyaelekeze daima macho yetu kwenye mbingu mpya na dunia mpya;
- utuwezeshe kuishughulikia kwa makini zaidi hali ya sasa na ya baadaye ya ulimwengu wetu. (W.)
Ulishuka kuzimu kuwapasha marehemu habari njema;
- uwakaribishe kwako waamini marehemu, wewe uliye furaha yao, matumaini yao, na utukufu wao. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana, isikie sala yetu. Umtume kwa watu wote Roho anayetufanya tuwe wana wako, kama alivyobashiri
Kristo, shahidi wa ukweli wako: na hivi uikamilishe, kwa njia ya injili, kazi ya kutakatifuza,
iliyoahidiwa na Neno wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.