Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 5 PASAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya

Zab.119:25-32 IV Mwongozo wa Mungu
Nagaagaa chini mavumbini,*
unipe tena uhai kama ulivyoahidi.

Nimeungama niliyotenda, nawe ukanisikiliza;*
unifundishe mwongozo wako.

Unifundishe namna ya kushika amri zako,*
nami nitayatafakari matendo yako ya ajabu.

Niko hoi kwa uchungu;*
unirudishie nguvu kama ulivyoahidi.

Uniepushe na njia ya upotovu;*
unijalie niijue sheria yako.

Nimechagua njia ya uaminifu;*
nimezingatia hukumu zako.

Ee Mungu, nimefuata maagizo yako;*
usikubali niaibishwe!

Nitafuata maagizo yako,*
maana unanipa maarifa zaidi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.26 Sala ya mtu mwema
Mungu ametuteua tuwe watu wake katika kuungana na Kristo, ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake (uf.1:4)

Ee Mungu, unitetee,/
maana nimeishi bila hatia,*
nakutumainia wewe bila kusita.

Unijaribu, Ee Mungu, na kunichunguza;*
upime moyo wangu na akili yangu.

Upendo wako mkuu waniongoza;*
nimeishi kufuatana na ukweli wako.

Siandamani na watu wapotovu;*
sishirikiani na watu wanafiki.

Nachukia kujumuika na wabaya;*
wala sitaandamana na waovu.

Nanawa mikono yangu, Ee Mungu,*
kuonyesha kwamba sina hatia;

najiunga na maandamano ya ibada,*
kuzunguka madhabahu yako,

nikiimba wimbo wa kukushukuru,*
na kutangaza matendo yako ya ajabu.

Ee Mungu, napenda makao yako,*
mahali unapokaa utukufu wako.

Usinipatilize pamoja na wenye dhambi,*
wala usinitupe pamoja na wauaji:

Watu ambao matendo yao ni maovu daima,*
watu ambao daima hula rushwa.

Lakini mimi hutenda yaliyo sawa;*
unihurumie na kunikomboa.

Kama nikiwa imara na salama,*
nitamsifu Mungu kati ya jamii kubwa ya watu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.28:1-3,6-9 Kuomba msaada
Nakushukuru Baba, kwa kuwa wewe wanisikiliza (Yoh.11:41)

Nakulilia, Ee Mungu, mwamba wa usalama wangu!/
Unisikilize, usiwe kama kiziwi kwangu;*
nisije nikawa kama wale washukao shimoni kwa wafu.

Unisikilize niombapo msaada,/
niinuapo mikono yangu,*
kuelekea mahali pako patakatifu.

Usinihukumu pamoja na watu wabaya,*
pamoja na watu watendao maovu:

watu wasemao maneno mazuri,*
kumbe wamejaa uhasama moyoni mwao.

Atukuzwe Mungu,*
maana amesikiliza ombi langu.

Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu;*
namtumainia yeye kwa moyo wangu wote.

Ananisaidia na kunifurahisha;*
nitamsifu kwa tenzi za shangwe.

Mungu ni nguvu ya watu wake;*
humkinga na kumwokoa mfalme wake mteule.

Ee Mungu, uwaokoe watu wako;/
uwabariki hao watu walio mali yako.*
Uwachunge na kuwalinda hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Mate.2:32,36
Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu, na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo. Ni lazima watu wote wa Israeli wafahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulibisha ninyi, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Masiha.

K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Gal.3:27-28
Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja katika kuungana na Kristo Yesu.

K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 1Kor.5:7,8
Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa sadaka. Basi, tufanye karamu hiyo sio kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na ukweli.

K. Kaa nasi,Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, ujalie, fumbo la Pasaka liyaunde maisha yetu, ili kile tunachoadhimisha kwa furaha, daima kitupatie ulinzi na wokovu. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.