IJUMAA JUMA LA 5 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.15:22-31
Siku zile, baada ya Mtaguso wa Yerusalemu, ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua
watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa
Barnaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao,
Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa;
Salamu. Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha
roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua
watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatarisha maisha
yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia
wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike
mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu,
na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo mtafanya vema. Wasalamu. Hata hao wakiisha
kupewa ruhusa wakatelemkia Antiokia; na baada ya kuwakusanyia jamii yote wakawapa ile barua. Nao
walipokwisha kuisoma, wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.57:7-11 (K)9
1. Ee Mungu, moyo wangu u thabiti,
Moyo wangu u thabiti.
Nitaimba, nitaimba zaburi,
Amka, utukufu wangu.
Amka, kinanda na kinubi,
Nitaamka alfajiri.
(K) Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu.
2. Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu,
Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni,
Na uaminifu wako hata mawinguni.
Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. (K)
SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu,
nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
INJILI: Yn.15:12-17
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi.
Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi
mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo
bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda;
na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru
ninyi, mpate kupendana.
MAOMBI
Ndugu wapendwa, Amri Kuu ya Mapendo inatudai kupendana kama Yesu alivyotupenda hata akawa tayari
kuutoa uhai wake kwa ajili ya sisi rafiki zake wakosefu. Ili tuweze kuiishi Amri hii Kuu kwa unyofu
wote, tunahitaji msaada wa Mungu. Tumwombe:
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Viongozi wa Kanisa wafanane zaidi na Mwanao katika kuutangaza upendo wako kwa maneno na matendo.
2. Kila kiongozi katika jamii akumbuke kuwa amechaguliwa na Mungu kwa njia ya watu, apate kutenda
aliyoamriwa na kuahidi mbele ya watu na Mungu aliye shahidi mwaminifu.
3. Kila mwanadamu ajijengee mazingira ya kuzuia utumwa ili kujenga urafiki wa kweli kati ya wakubwa
na wadogo.
4. Mwanao aliyetoa uhai wake kwa ajili yetu, sasa kwa huruma yake awapokee kirafiki katika ufalme
wake ndugu zetu marehemu.
Ee Baba Mwema, Mwanao ametukumbusha kwamba siyo sisi tuliomchagua yeye, bali ni yeye aliyetuchagua
sisi na akatuweka duniani tupate kuzaa matunda, na matunda yetu yapate kukaa. Utujalie neema yako
tupate kuyatimiza hayo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.