Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 5 PASAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!

Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!

Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!

Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534

2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ

3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.

Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876

4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.

Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.

Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.

Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.

Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.

Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.

Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.

Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7

5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.

Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.

Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.

Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.

Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750

7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.

Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.

Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.

Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.

Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695

ANT. I: Kristo amejifanya fukara, ili sisi tupate utajiri, aleluya.

Zab.41 Sala ya mgonjwa
Mmoja wenu, anayekula pamoja nami, atanisaliti (Mk.14:18)

Heri mtu anayewashughulikia maskini,*
Mungu atamsaidia wakati wa shida.

Mungu atamlinda na kumweka hai;/
atamfanikisha katika nchi;*
hatamwacha katika makucha ya adui zake.

Mungu atamsaidia awapo mgonjwa;*
na kumpatia nafuu ya maradhi yake.

Nami nilisema: "Nimekukosea wewe, Ee Mungu,*
unihurumie ukaniponye."

Adui zangu husema mabaya juu yangu;*
wanataka nife na kusahauliwa kabisa.

Wanitembeleapo huwa hawana nia njema;/
wanawaza mabaya juu yangu,*
wafikapo nje huwatangazia wengine.

Wote wanichukiao hunong'onezana juu yangu;*
waniwazia mabaya ya kunidhuru.

Husema: “Maradhi haya yatamwua;*
hatatoka tena kitandani mwake!“

Hata rafiki yangu mkuu ambaye nilimtegemea,/
ambaye alishiriki chakula changu,*
amegeuka na kuanza kunishambulia!

Ee Mungu, unionee huruma!*
Unipe nafuu, nami nitawalipiza.

Hivyo nitajua kwamba umenifadhili,*
ikiwa adui zangu hawatanishinda.

Utanitegemeza, kwani natenda yaliyo sawa;*
utaniweka mbele yako milele.

Asifiwe Mungu, Mungu wa Israeli!*
Asifiwe sasa na milele!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Kristo amejifanya fukara, ili sisi tupate utajiri, aleluya.

ANT. II: Maji ya mto yaufurahisha mji wa Mungu, aleluya.

Zab.46 Mungu yuko upande wetu
Naye ataitwa Emanueli (maana yake, "Mungu yuро рamoја nasi") (Mt.1:23)

Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu;*
yu tayari daima kusaidia wakati wa taabu.

Kwa hiyo hatutaogopa chochote,*
dunia ijapoyeyuka na milima kuanguka baharini;

hata kama bahari ikichafuka na kutisha,*
na vilima vikatikiswa kwa shambulio lake.

Kuna mto ambao maji yake yaufurahisha mji wa Mungu,*
makao matakatifu ya Mungu Mkuu.

Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa;*
alfajiri na mapema huuletea msaada.

Mungu anguruma, dunia yayeyuka;*
mataifa yaghadhabika na tawala zatikisika.

Mwenyezi mwenye nguvu, yu pamoja nasi,*
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

Njoni mkaone matendo makuu ya Mungu;*
oneni maajabu aliyoyafanya duniani.

Hukomesha vita popote duniani,/
huvunjavunja pinde na mikuki,*
nayo magari ya vita huyateketeza.

Asema: “Nyamazeni!*
jueni kwamba mimi ndimi Mungu!

Mimi natukuzwa na mataifa yote;*
mimi ni mkuu wa ulimwengu wote!"

Mungu, Mungu mwenye nguvu, yu upande wetu,*
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Maji ya mto yaufurahisha mji wa Mungu, aleluya.

ANT. III: Tumwimbie Bwana, kwa kuwa ushindi wake ni mkuu, aleluya.

WIMBO: Ufu.15:3-4. Utenzi wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!

Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!

Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.

Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina.

Ant. III: Tumwimbie Bwana, kwa kuwa ushindi wake ni mkuu, aleluya.

SOMO: Ebr.5:8-10
Ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kwa njia ya mateso kutii. Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii, naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.

KIITIKIZANO
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Walipomwona Bwana.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wanafunzi...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko ule wa mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko ule wa mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake, aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Kristo, ambaye ni njia, ukweli na uzima.
W. Mwana wa Mungu aliye hai, uwabariki watu wako.

Tunawaombea watumishi wote wa Kanisa lako:
- wanapowagawia ndugu zao chakula cha uzima, wao wenyewe washibishwe na kuimarika. (W.)

Tunawaombea Wakristo wote:
- wawe waaminifu kwa wito wao, na washikilie na kudumisha umoja wa kiroho, wakishirikiana kwa amani. (W.)

Tunawaombea watawala wa nchi yetu, wapate kutumia madaraka yao kwa haki na huruma;
- uwasaidie waweze kukuza amani duniani. (W.)

Utufanye tustahili kukuabudu wewe tukishirikiana na watakatifu;
- uwajalie furaha ya milele waamini marehemu, ambao tunawaweka mikononi mwako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, ujalie, fumbo la Pasaka liyaunde maisha yetu, ili kile tunachoadhimisha kwa furaha, daima kitupatie ulinzi na wokovu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.