IJUMAA JUMA 5 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Yer.20:10-13
Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite,
husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake.
Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa,
wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele,
ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno
na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu. Mwimbieni
Bwana; msifuni Bwana; kwa maana ameiponya roho ya mhitaji katika mikono ya watu watendao maovu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.18:1-6
1. Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu,
Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia,
Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa,
Hivyo nitaokoka na adui zangu.
(K) Katika shida yangu nalimwita Bwana,
akaisikia sauti yangu.
2. Kamba za mauti zilinizunguka,
Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
Kamba za kuzimu zilinizunguka,
Mitego ya mauti ikanikabili. (K)
3. Katika shida yangu nalimwita Bwana,
Na kumlalamikia Mungu wangu.
Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake,
Kilio change kikaingia masikioni mwake. (K)
SHANGILIO: 2Kor.5:19
Mbegu ni neno la Mungu,
mpanzi lakini ni Kristu,
yeyote ampataye, ataishi milele.
INJILI: Yn.10:31-42
Wayahudi waliokota mawe ili wampige. Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonesha zitokazo
kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe? Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili
ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya
mwenyewe u Mungu. Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema,
Ndinyi miungu? Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka);
je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema,
Mimi ni Mwana wa Mungu? Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa
hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni
ndani ya Baba. Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao. Akaenda zake tena ng’ambo ya
Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohane akibatiza hapo kwanza, akakaa huko. Na watu wengi
wakamwendea, wakasema, Yohane kweli hakufanya ishara yoyote, lakini yote aliyoyasema Yohane katika
habari zake huyu yalikuwa kweli. Nao wengi wakamwamini huko.
MAOMBI
Ndugu, Yesu ni Mungu-mtu na Masiha wetu. Tumwombe ili, tunapomtangaza kuwa ndiye aliyeteswa, akafa, akazikwa na
siku ya tatu akafufuka, watu wote duniani waupokee ukweli huo. Ee Bwana Yesu.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Watangazaji wote wa Injili yako wasihofu kukuhubiri wewe sababu ya mashutumu ya watu.
2. Uwe pamoja na wote wanaoviziwa na kushitakiwa kwa uwongo kwa sababu ya imani yao kwako; na uziponye
roho zao.
3. Uwajalie waamini wote kuzitenda kazi njema zitokazo kwa Baba yako, ili ulimwengu wote upate kuokoka.
4. Utukinge na kufuru ya aina yoyote dhidi yako wewe na Baba na Roho Mtakatifu, ili tuwe kweli ndani ya
Baba na Baba awe ndani yetu.
Ee Bwana, ingawa Wayahudi walitaka kukupiga mawe, wengi walikukiri kuwa Wewe ni Mkuu kuliko Yohane Mbatizaji,
wakakuamini. Utudumishe katika imani kwako na kwa kazi yako ya ukombozi. Unayeishi na kutawala, daima na milele. Amina.