IJUMAA JUMA 4 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Hek.2:1,12-22
Wasiomsadikia Mungu walisema hivi, huku wakimfikiri yasiyo kweli, Zaidi ya hayo na tumwotee
mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu; atukaripia ya kama
tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu. Asema ya kwamba anamjua Mungu, na
kujiita mtumishi wa Bwana. Ametuwia magombezi ya fikira zetu. Hata kumtazama twaona ni kugumu;
maana amaisha yake si sawasawa na maisha ya wengine, na mwenendo wake ni wa kigeni. Tunahesabiwa
naye kuwa kama madini hafifu; anajitenga na njia zetu kama na uchafu. Wenye haki asema kuwa
mwisho wao ni heri; hujivuna ya kwamba Mungu ndiye baba yake. Haya na tuone kama maneno yake
ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; mradi mwenye haki akiwa ni
mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa
jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata
tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake. Ndivyo walivyosemezana,
wakakosea kabisa. Kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu; wala hawakuutarajia
mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:16-20,22(K)18
1. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana kasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
(K) Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo.
2. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini Bwana humponya nayo yote. (K)
3. Huihifadhi mifupa yake yote,
Haukuvunjika hata mmoja.
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)
SHANGILIO: Lk.8:15
Heri wale walishikao neno la Mungu
katika moyo wao mwema na mnyofu,
na wazaao matunda katika uvumilivu.
INJILI: Yn.7:1-2,25-30
Baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi,
kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda,
ilikuwa karibu. Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea,
si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri. Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu
siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao
wakuu tuna jua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo
atakapokuja hakuna ajuaye atokako. Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na
kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye
aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye
aliyenituma. Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika,
kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.
MAOMBI
Ndugu zangu, saa ya kutukuzwa Mwana wa Mtu inazidi kukaribia. Kwa kuwa mateso yake ni kwa ajili yetu, tuombe
huruma yake. Ee Bwana Yesu, twakuomba:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwahurumie wote wanaoiga tabia ya Wayahudi ambao hawakutaka kukupokea kama Mkombozi wao uliyetumwa na Mungu.
2. Uwasamehe wote wanaowakosea haki viongozi wetu wa Kanisa kwa dhihaka, matusi na majungu.
3. Uwarehemu wote wanaoteswa kwa ajili ya kulieneza neno lako, na uwape nguvu ya kuubeba msalaba huo mpaka siku
ya ukombozi wao.
4. Usiwahesabie makosa yao marehemu wetu, ili wafufuke pamoja nawe na kushiriki uzima mpya.
Tunaomba hayo yote kwako wewe Mtumishi wa Bwana unayeishi na kutawala na Baba na Roho Mtakatifu, Mungu, daima
na milele. Amina.