IJUMAA JUMA LA 3 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.9:1-20
Siku zile, Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu,
akataka ampe barua za kwenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii,
waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hapo alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia
Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti
ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi
Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale
watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. Sauli akainuka
katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski.
Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. Basi palipokuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania.
Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. Bwana akamwambia, Simama, enenda
zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana,
angalia, anaomba; naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate
kuona tena. Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi
aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge
wote wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu,
alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonesha yalivyo
mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu. Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani,
akamwekea mikono akisema, Ndugu, Sauli, Bwana amenituma, Yesu yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia,
upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata
kuona, akasimama, akabatizwa, akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja
na wanafunzi walioko Dameski. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.117(K)Mk.16:15
1. Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini.
(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
2. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SHANGILIO: Rum.6:9
Aleluya, aleluya,
Kristo akiisha kufufuka katika
wafu hafi tena,
wala mauti haimtawali tena.
Aleluya.
INJILI: Yn.6:52-59
Siku ile, Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake
ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu
na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima
wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu
yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami
hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika
naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si
kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. Maneno hayo aliyasema
katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu.
MAOMBI
Ndugu, kwa kuongoka kwa Saulo na kwa tendo la Yesu kujifanya chakula cha roho zetu, tunakumbushwa
ukweli huu kwamba hakuna lisilowezekana kwa Mungu, na kwamba tunapaswa kumtegemea Mungu daima.
Kwa hiyo, tuombe:
Kiitikio: Kwa huruma yako Bwana, utusikie.
1. Uwakinge na hila za adui viongozi wetu wa Kanisa.
2. Ubariki juhudi za viongozi wa serikali na wote wenye mamlaka wanaotumia kila njia halali
kupambana na maovu duniani.
3. Uwasaidie wote wanaoenda kinyume na Neno lako waongoke kwa mfano wa Mt. Paulo mtume.
4. Utuondolee woga katika utume wetu na uwashirikishe marehemu wetu maisha ya ufufuko wa Mwanao.
Kwa vile hakuna lisilowezekana kwako, Ee Mungu, utujalie udumifu katika kuyaadhimisha haya
mafumbo yako matakatifu tupate kuyatangaza mauti ya Mwanao mpaka ajapo. Kwa njia ya huyo Kristo
Bwana wetu. Amina.