IJUMAA JUMA 33 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Mak.4:36-37,52-59
Yuda na ndugu zake walisema, Sasa adui zetu wamevunjwa nguvu, basi tupande tukapatakase mahali
patakatifu na kupatabaruku. Jeshi lote likakusanyika likapanda juu ya mlima Sayuni. Wakaondoka
mapema siku ya ishirini na tano ya mwezi wa tisa, yaani Kislevu, mwaka mia arobaini na nane,
wakatoa dhabihu, kama ilivyoamriwa katika sheria, juu ya madhabahu mpya ya sadaka za kuteketezwa
waliyokuwa wameifanya. Wakati ule ule na siku ile ile iliyotiwa unajisi na mataifa, siku ile ile
iliwekwa wakfu tena kwa nyimbo na vinubi na vinanda na matari. Watu wote wakaanguka kifudifudi
wakipaza sifa kwa mbingu, kwake aliyewapa ufanisi. Wakaiadhimisha sikukuu ya kuitabaruku madhabahu
muda wa siku nane, wakileta sadaka za kuteketezwa kwa furaha na kutoa dhabihu ya wokovu na shukrani.
Pia, waliupanda ukuta wa mbele wa hekalu kwa taji za dhahabu na vigao; wakaweka wakfu malango na
vyumba vya makuhani na kuvitia milango. Kulikuwa na furaha kubwa kwa watu, na aibu iliyoletwa na
mataifa iliondolewa. Yuda na ndugu zake, na jamii yote ya Israeli, walikata shauri ya kuwa siku
za kuitabaruku madhabahu ziadhimishwe kwa furaha na shangwe kila mwaka kwa wakati wake, muda wa
siku nane tangu ishirini na tano ya mwezi Kislevu.
WIMBO WA KATIKATI: Nya.29:10-12 (K)13
1. Uhimidiwe, Ee Bwana,
Mungu wa Israeli baba yetu,
Milele na milele.
(K) Tulisifu jina lako tukufu, Ee Bwana.
2. Ee Bwana, ukuu ni wako,
Na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi.
Utajiri na heshima hutoka kwako. (K)
3. Wewe watawala juu ya vyote,
Na mkononi mwako mna uweza na nguvu,
Tena mkononi mwako mna kuwatukuza,
Na kuwawezesha wote. (K)
SHANGILIO: Yn.15:15
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema:
Siwaiti tena watumwa,
lakini ninyi nimewaita rafiki,
kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya!
INJILI: Lk.19:45-48
Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa,
Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Naye akawa
akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa
wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye,
wakimsikiliza.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, tupeleke sasa maombi yetu kwa Mungu anayependa tuitumie vema nyumba yake ya
sala kwa manufaa yetu sisi wenyewe.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Maaskofu na Mapadre wetu wasichoke kutolea dhabihu ya wokovu na shukrani
altareni pako. Ee Bwana.
2. Watawala wote duniani wajenge mazingira rafiki kwa uenezaji Injili na utoaji
unabii juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi. Ee Bwana.
3. Wote wakuaminio wakuabudu kifudifudi, wakipaza sifa mbinguni,
kwako Wewe unayewafanikisha katika maisha. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote kushika kiaminifu na kitakatifu Siku yako Bwana,
na Sikukuu zote ulizotuamuru kwa ajili ya wokovu wetu. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wapate kitulizo na faraja, kwa kusamehewa
dhambi na kupewa uzima wa milele. Ee Bwana.
Ee Mungu, uyapokee maombi haya tuliyokutolea. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.