IJUMAA JUMA 32 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Hek.13:1-9
Bila shaka wanadamu wote kwa asili ni ubatili, ambao hawana akili za kumtambua Mungu; tena hawakupata uwezo wa kumjua yeye aliopo kwa kuvitazama viumbe vizuri vinavyoonekana, wala kwa kuyaangalia yaliyofanywa hawakufahamu yule fundi aliyeyafanya. Walakini moto, ama upepo, ama hewa nyepesi, ama mzunguko wa nyota, ama mafuriko ya maji, ama mianga ya mbinguni walidhania kuwa ni miungu inayoutawala ulimwengu! Huenda ilikuwa kwa kupendezwa na uzuri wake walivyodhania viumbe hivyo kuwa ni miungu, basi na wajue kadiri gani Bwana, Mfalme wao avipitiavyo; kwa maana yeye aliye asili ya uzuri ndiye aliyeviumba. Lakini kama ilikuwa kwa kuzistaajabia nguvu zake na maongozi yake, na wafahamu kwa kuviangalia kadiri gani yeye aliyeviumba anayo nguvu zaidi; maana kwa jinsi uzuri hata wa viumbe vilivyoumbwa ulivyo mkuu, kwa kadiri iyo hiyo mwanadamu huyatunga mawazo yake juu ya Muumba. Walakini watu hao hawana hatia nyingi. Madhali yawezekana kwamba hao wamekosea tu, pindi wanapomtafuta Mungu, na kutamani kumwona; kwa sababu huishi katikati ya viumbe vyake, huvichunguza kwa bidii, na mwisho hujitoa kwa maono yao, mradi vitu vyenyewe wanavyovitazama ni vizuri kweli kweli. Walakini tena watu hao hawana udhuru. Kwa maana ya viumbe, imekuwaje ya kwamba hawakudiriki upesi kumtambua Mfalme Mkuu wa viumbe hivyo vyake?

WIMBO WA KATIKATI: Zab.19:1-4 (K)1
1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa.

(K) Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu.

2. Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani. Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. (K)

SHANGILIO: Zab.111:7,8
Aleluya, aleluya!
Maagizo yako yote, Ee Bwana, ni amini,
yamethibitika milele na milele.
Aleluya!

INJILI: Lk.17:26-37
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulikunya moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu yeyote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na yeyote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia. Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Mwanao amesema ulipo mzoga ndipo watakapokutanika tai. Sisi tuliokusanyika hapa kwa jina lake, twakuomba:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Viongozi wetu wa Kanisa wasichoke kuwakumbusha watu wako juu ya ujio wa Mwanao siku ya mwisho. Ee Bwana.

2. Utawale mioyo ya viongozi wote wa serikali, ili wasiruhusu nchini dini haramu au vikundi vya matapeli na wadanganyifu; bali wasimamie utu wema, haki, ukweli na amani. Ee Bwana.

3. Wote wasiokufahamu wapate kukiri uwepo wako, walao kwa kuvitazama viumbe vizuri vinavyoonekana, na kwa kuzichungulia taratibu za viumbe hivyo. Ee Bwana.

4. Sisi tunaomwamini Mwanao Yesu Kristo tujaliwe kuikiri imani yetu kwa maneno na matendo yetu mema siku zote. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na kufikishwa kwako huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tuwe tayari hata kuziangamiza nafsi zetu kwa ajili yako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.