IJUMAA JUMA 31 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.15:14-21
Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa
elimu yote, tena mwaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu,
kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya
watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali,
ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za
Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa
neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu
Yerusalemu, na kando kando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu;
kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa,
nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine; bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiohubiriwa habari
zake wataona, Na wale wasiojasikia watafahamu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-4 (K)2
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake. (K)
3. Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu. (K)
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: Mimi ndimi njia,
na ukweli, na uzima,
mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!
INJILI: Lk.16:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu
alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia
juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena. Yule wakili akasema moyoni
mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua
nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao. Akawaita wadeni wa
bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? Akasema, Vipimo mia vya mafuta.
Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini. Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani?
Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini. Yule bwana akamsifu wakili
dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa
na busara kuliko wana wa nuru.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa unyenyekevu na unyofu wa moyo,
tumwombe Mungu katika shida zetu.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu
na Mapadre wetu wote waifanyie Injili yako kazi ya ukuhani, kusudi
Mataifa wawe sadaka yenye kibali mbele yako. Ee Bwana.
2. Wote waliodhaminiwa kazi ya utunzaji mali kwa niaba
ya wengine katika jamii, wajaliwe kuifanya kazi hiyo kwa busara
yenye kuhesabiwa haki. Ee Bwana.
3. Utujalie unyenyekevu, tupate kutambua uwepo wako
wa daima katika shughuli zetu za kila siku, na tuone fahari
kuitukuza kazi yako. Ee Bwana.
4. Uimarishe utashi wetu dhidi ya maadui wa Msalaba
wa Mwanao, Yesu Kristo; ili fahari yetu iwe katika kuacha anasa
za dunia zinazopingana na wenyeji wetu huko mbinguni. Ee Bwana.
5. Uwakaribishe ndugu zetu marehemu katika ufalme
wako wa mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka unyofu wa moyo katika mahusiano yetu, uyapokee
maombi haya. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.