IJUMAA JUMA 30 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.9:1-5
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba
nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe
niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao
ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya
Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye
aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.147:12-15,19-20 (K)12
1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako.
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
2. Ndiye afanyaye Amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana. (K)
3. Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua.
Aleluya. (K)
SHANGILIO: Zab.119:34
Aleluya, aleluya,
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya.
INJILI: Lk.14:1-6
Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato,
ale chakula, walikuwa wakimvizia. Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura.
Yesu akajibu, akawaambia wanasheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama
sivyo? Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. Akawaambia, Ni nani miongoni
mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya
sabato? Nao hawakuweza kujibu maneno haya.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Yesu Kristo ni tabibu wa mwili na roho na
sheria yake huleta uhuru. Tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu na viongozi wote
wa Kanisa wasiwaonee haya wanaolikejeli jina lako,
bali wadumu katika kuwatangazia ukweli wako. Ee Bwana.
2. Pendo, hekima, haki na ufahamu wa viongozi wa
serikali kwa raia wao vizidi kukua; wapate
kuyakabili yaliyo mema kadiri ya mapenzi yako. Ee Bwana.
3. Watu wote wajaliwe kukukiri kuwa Wewe ndiwe
tabibu wa kweli na Mwana wa Mungu, aliye juu
ya mambo yote na mwenye kuhimidiwa milele. Ee Bwana.
4. Kwa huruma yako, utuponye na magonjwa yetu
mbalimbali, hata yale yaliyojificha ndani mwetu au
yasiyotambulika kwa matabibu. Ee Bwana.
5. Uwape msamaha wa dhambi ndugu zetu marehemu,
wapate kuhesabiwa katika kundi la wana wa Mungu
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Yesu, mponyaji mwili na roho, uyapokee maombi
yetu. Unayeishi na kutawala daima na milele. Amina.