IJUMAA JUMA LA 2 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo 5:34-42
Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu
wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume
wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka
Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa
na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya,
siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na
wote waliomsadiki wakatawanyika. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa
kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa
Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu. Wakakubali maneno yake; nao
walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende
zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa
kwa ajili ya Jina hilo. Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na
kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.27:1,4,13-14(K)4
1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nikae nyumbani mwa Bwana.
2. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)
3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
SHANGILIO: Zab.118:24
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa na Kristo,
yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko,
ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
INJILI: Yn.6:1-15
Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na
mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa. Naye Yesu akakwea
mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Na Pasaka, sikukuu ya Wayahudi, ilikuwa karibu.
Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue
wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe
atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo
tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna
mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu
akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi,
wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi;
na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka. Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi
wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote. Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu
kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula. Basi watu
wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni.
Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, akajitenga,
akaenda tena mlimani yeye peke yake.
MAOMBI
Ndugu zangu, leo tunakumbushwa kwamba ikiwa kazi imetoka kwa binadamu peke yake, itavunjwa,
lakini ikiwa imetoka kwa Mungu haiwezi kuvunjwa. Kwa hiyo tuombe, ili mapenzi yake yatimizwe.
Kiitikio: Bwana utusikie, Bwana utusikilize.
1. Maaskofu na mapadre ambao ni warithi wa mitume wadumu katika kulichunga na kulilisha kundi
lako ulilowakabidhi.
2. Hata leo utuinulie walimu, wanasheria na waamuzi wenye busara kama Gamalieli, ili tudumishe
uhuru, haki, amani na usawa.
3. Wafuasi wote wa Kristo tusiogope kuteswa kwa ajili ya Kristo na, inapotokea, daima tufurahie
kushiriki kazi ya ukombozi kwa njia ya mateso.
4. Kwa ushindi aliotupatia Mwanao dhidi ya shetani, dhambi na mauti, uwainue marehemu mpaka huko
juu mbinguni.
Ee Bwana Mungu, wewe ni kimbilio la wote wanaoteseka pia chanzo na kikomo cha furaha ya kweli.
Fumbo la Paska lizidi kututhibitishia ukweli huu kila tunapoliadhimisha. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.