IJUMAA JUMA 29 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Rum.7:18-25
Najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:66,76-77,93-94 (K)68
1. Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako.

(K) Unifundishe akili na maarifa, Ee Bwana.

2. Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. (K)

3. Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu. (K)

4. Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha. (K) 5. Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako. (K)

SHANGILIO: 2.Kor.5:19
Aleluya, aleluya!
Mungu alikuwa ndani ya Kristo,
akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake,
ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya!

INJILI: Lk.12:54-59
Yesu aliwaambia makutano pia, kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo. Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya? Na mbona ninyi wenyewe kwa nafsi zenu hamwamui yaliyo haki? Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidi kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani. Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa kwake yeye atakaye kutenda lililo jema lipo baya lisilotakiwa, tuombe neema ya Mungu.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili Askofu wetu F. na wahubiri wote wa neno lako wasichoke kukemea maovu na kuhamasisha matendo mema yaletayo uzima wa milele. Ee Bwana.

2. Ili hata watawala wa dunia watambue kuwa amani ya kweli hutokana na kufurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani. Ee Bwana.

3. Ili, kwa kuepukana na unafiki, tuokolewe na mauti yaletwayo na mambo ya kimwili. Ee Bwana.

4. Ndugu, marafiki na wana ndoa waliofarakana, wajirudi na kuenenda inavyostahili wito wao kwa unyenyekevu; wakichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Ee Bwana.

5. Ili ndugu zetu waliofariki dunia wafike kwako mbinguni na kufurahi nawe milele. Ee Bwana.

Ee Mungu Baba uliyekubali Mwanao afe msalabani japo hakuwa na kosa lolote, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.