IJUMAA JUMA 28 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.4:1-8
Tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili? Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki
kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu. Maana maandiko yasemaje?
Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki. Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake
hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni. Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye
ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, Imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. Kama vile Daudi
aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo, Heri waliosamehewa
makossa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.32:1-2.5.11 (K)7
1. Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makossa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
Ambaye rohoni mwake hamna hila.
(K) Ni wewe sitara yangu, Ee Bwana.
2. Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. (K)
3. Mfurahieni Bwana;
Shangilieni, enyi wenye haki.
Pigeni vigelegele vya furaha;
Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo. (K)
SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana,
na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.
INJILI: Lk.12:1-7
Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake
kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki. Lakini hakuna neno lililositirika
ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana. Basi, yoyote mliyosema gizani
yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya
dari. Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana
wawezalo kutenda Zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa, mwogopeni yule ambaye akiishakumwua
mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanam; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo. Je! Mashomoro watano
hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za
vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa kwa Mungu hakuna neno lililositirika
ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo
halitajulikana, tuombe neema yake:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Ili Maaskofu na viongozi wote wa Kanisa lako
wapate kuhesabiwa haki, kwa ajili ya kazi ya
kulichunga kundi lako hapa duniani. Ee Bwana.
2. Uwajalie viongozi wa serikali kukuogopa Wewe
Mungu, na kufanya mambo yote ya utawala kwa
shauri la mapenzi yako, ili raia wote tuwe warithi
wa raslimali ulizotujalia. Ee Bwana.
3. Ili watu wote wakutumainie Wewe Mungu mwenye
uwezo wa kuokoa mwili na roho. Ee Bwana.
4. Ili kila mmoja wetu aepukane na unafiki, kwa kutenda
matendo ya mwanga yanayoonekana na kukubalika na wote. Ee Bwana.
5. Ili marehemu wetu, wakiisha kusamehewa dhambi zao
kadiri ya mapenzi yako, wafikishwe kwako mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetupenda na kututhamini zaidi sisi kuliko
mashomoro wengi, uisikilize sala yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.