IJUMAA JUMA 27 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Yoe.1:13-15,2:1-2
Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku
kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji
Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye
wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa Bwana, Mungu wenu, Na kumlilia Bwana, Ole wake siku hii!
Kwa maana siku ya Bwana inakaribia, nayo itakuja kama uangamivu utokao kwake aliye Mwenyezi. Pigeni
tarumbeta katika Sayuni, Pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu; Wenyeji wote wa nchi na
watetemeke; Kwa maana siku ya Bwana inakuja. Kwa sababu inakaribia; siku ya giza na weusi, siku
ya mawingu na giza kuu. Kama mapambazuko yakitandazwa juu ya milima, hao ni wakuu, tena wenye
nguvu, mfano wao haukuwako kamwe, wala hautakuwako baada ya hao, hata katika miaka ya vizazi vingi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.9:1-2,5,15,7-8 (K)8
1. Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote;
Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;
Nitafurahi na kukushangilia Wewe;
Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu.
(K) Bwana atahukumu ulimwengu kwa haki.
2. Umewakemea mataifa;
Na kumwangamiza mdhalimu;
Umelifuta jina lao milele na milele;
Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya;
Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao. (K)
3. Bali Bwana atakaa milele,
Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu.
Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki;
Atawaamua watu kwa adili. (K)
SHANGILIO: 1The.2:13
Aleluya, aleluya!
Lipokeeni neno la Mungu,
siyo kama neno la wanadamu,
bali kama neno la Mungu.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:15-26
Wengine wa makutano walisema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu,
wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia. Kila ufalme uliofitinika
wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa shetani naye
amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa
pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani?
Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu,
basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo
nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda,
amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja
nami yu kinyume changu; na mtu aliyekusanya pamoja nami hutawanya. Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia
mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitarudia nyumba yangu niliyotoka.
Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu
kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya
kwanza.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Yesu umesema: “Mtu ambaye si pamoja nami yu
kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami
hutawanya.” Basi tunakuomba.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu
na viongozi wote wa Kanisa wabaki imara, katika kuifundisha
na kuitetea imani sahihi, dhidi ya waasi na wanaolikufuru jina
lako. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka katika jamii wawe chachu
nzuri, wapate kuigwa na watu wao katika kujiandaa
kwa siku ya ujio wako. Ee Bwana.
3. Utuepushe na pepo wabaya na, kwa nguvu ya Roho wako
Mtakatifu, utuimarishe katika kupambana na maadui wa imani
yetu kwako. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wenye imani haba, ili waepukane na
dhambi ya kumkufuru Roho wako Mtakatifu; wala wasiwakwaze
wanyofu wa moyo. Ee Bwana.
5. Wote waliofariki dunia watakaswe dhambi zao na
kufikishwa huko kwako mbinguni. Ee Bwana.
Ee Yesu uliyetupenda mpaka kufa, uyapokee maombi
yetu. Unayeishi na kutawala daima na milele. Amina.