IJUMAA JUMA 26 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Bar.1:15-22
Kwa Bwana Mungu wetu, haki; lakini kwetu sisi haya ya uso kama hivi leo, kwa watu wa Yuda na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa wafalme wetu, na kwa wakuu wetu, na kwa makuhani wetu, na kwa manabii wetu, na kwa baba zetu, kwa sababu tumetenda dhambi mbele ya Bwana. Tumemwasi, wala hatukuitii sauti ya Bwana Mungu wetu, kwenda katika sheria zake alizoziweka mbele yetu. Tangu siku Bwana aliyowatoa baba zetu katika nchi ya Misri hata leo tumemwasi Bwana Mungu wetu na kutenda yasiyofaa kwa kutoisikiliza sauti yake. Kwa hiyo mapigo haya yameshikamana nasi, na ile laana ambayo Bwana alimwamuru mtumishi wake Musa, katika siku aliyowaleta baba zetu kutoka katika nchi ya Misri ili atupe nchi ijaayo maziwa na asali, kama hivi leo. Lakini hatukuisikiliza sauti ya Bwana Mungu wetu, kwa kuyafuata maneno yote ya manabii aliyotupelekea, bali tulikwenda kila mtu katika mawazo ya moyo wake mbaya, kutumikia miungu ya kigeni na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana Mungu wetu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.79:1-6,8-9 (K)9
1. Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako,
Wamelinajisi hekalu lako takatifu.
Wamefanya Yerusalemu chungu chungu.
Wameziacha maiti za watumishi wako
Ziwe chakula cha ndege wa angani.
Na miili ya watauwa wako
Iwe chakula cha wanyama wa nchi.

(K) Utusaidie, Ee Mungu,
kwa ajili ya utukufu wa jina lako.

2. Wamemwaga damu yao kama maji
Pande zote za Yerusalemu,
Wala hapakuwa na mzishi.
Tumekuwa lawama kwa jirani zetu,
Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira milele?
Wivu wako utawaka kama moto? (K)

3. Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu, Rehema zako zije kutulaki hima.
Kwa maana tumedhilika sana. (K)

4. Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K)

SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu,
nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!

INJILI: Lk.10:13-16
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.

--------------

--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu ametupatia Wachungaji katika Kanisa wapate kutuongoza badala yake. Tuombe neema yake Mungu tukisema.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Maaskofu, Mapadre na Makatekista wetu wazidi kutangaza msamaha wako, ili wakosefu waache njia zao mbaya na kukurudia Wewe, Mungu msamehevu. Ee Bwana.

2. Uwe pamoja na viongozi wa serikali, hasa wale wanaohitaji msaada wako, katika kukabiliana na changamoto za kiutawala, kwa manufaa ya raia wao na taifa zima. Ee Bwana.

3. Waamini wawe wasikivu kwa viongozi wao wa dini ili, kwa njia yao, wapate kukutana nawe, kukujua zaidi na kukutumikia kwa uchaji. Ee Bwana.

4. Umjalie kila mmoja wetu moyo wa toba, tupate kutubu dhambi zetu, kukusudia kuziacha na kuwasamehe wenzetu. Ee Bwana.

5. Kwa huruma yako, ndugu zetu marehemu wapewe uzima mpya huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uyapokee maombi haya na yale ambayo hatukuyataja. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.