IJUMAA JUMA 24 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Tim.6:2-12
Mambo hayo uyafundishe na kuonya. Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno
yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna; wala hafahamu
neno lolote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo
hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya; na majadiliano ya watu walioharibika akili zao,
walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. Walakini utauwa pamoja na
kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila
tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika
majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu
na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani
hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo
hayo; ukafuate haki, utauwa, Imani, upendo, saburi, upole. Piga vita vile vizuri vya Imani; shika
uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.49:5-9,16-19 (K)Mt.5:3
1. Kwa nini niogope siku za uovu,
Ubaya ukinizunguka miguuni pangu?
Wa hao wanaozitumainia mali zao,
Na kujisifia wingi wa utajiri wao.
(K) Heri walio maskini war oho,
maana ufalme wa mbinguni ni wao.
2. Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake,
Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake,
Maana fidia ya nafsi zao ina gharama,
Wala hana budi kuiacha hata milele.
Ili ishi sikuzote asilione kaburi. (K)
3. Usiogope mtu atakapopata utajiri
Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
Maana atakapokufa hatachukua chochote;
Utukufu wake hautashuka ukimfuata. (K)
4. Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai,
Na watu watakusifu ukijitendea mema,
Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake,
Hawataona nuru hata milele. (K)
SHANGILIO: Zab.19:8
Aleluya, aleluya!
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Aleluya!
INJILI: Lk.8:1-3
Yesu alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema
ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao
walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa
na pepo saba, na Yohana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa
wakimhudumia kwa mali zao.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, twakiri kuwa utaua pamoja na kuridhika ni
faida kubwa. Kwa vile tunasongwa na vishawishi na
magumu mengi katika maisha haya, tunathubutu kukuomba
tukisema.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwawezeshe viongozi wetu wa Kanisa kuvipiga vita
vile vizuri vya imani, na hivi kuwatia moyo waamini
wao katika kuilinda imani na kuyashinda majaribu. Ee Bwana.
2. Wote wanaotoa huduma kwa jamii wajaliwe kufuata
haki, upendo, saburi na upole. Ee Bwana.
3. Utuepushe sisi sote na tamaa ya fedha ambayo ni shina
la uharibifu na hatarishi kwa imani. Ee Bwana.
4. Kwa ajili ya wenye mashaka juu ufufuo wa wafu,
ili waongoke kutoka dhambini na kumwendea
Kristo aliye limbuko lao waliolala. Ee Bwana.
5. Uwajalie ndugu zetu marehemu uzima wa milele
walioitiwa wakiwa tangu hapa duniani. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetaka msalaba uwe alama ya ushindi wa
Mwanao, Yesu Kristo, dhidi ya dhambi, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu.
Amina.