IJUMAA JUMA 23 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: 1Tim.1:1-2,12-14
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu; kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.16:1-2,5,7-8,11 (K)5
1. Kwa maana nakukimbilia Wewe. Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; Sina wema ila utokao kwako. Bwana ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu.

(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.

2. Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku. Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)

3. Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele. (K)

SHANGILIO: Mt.4:4
Aleluya, aleluya!
Yesu akamjibu, “Imeandikwa:
‘Mtu haishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno asemalo Mungu.’”
Aleluya!

INJILI: Lk.6:39-42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenye huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafikiri wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, wema haupaswi kuuzidi uwezo. Ndiyo maana kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake. Tumwombe Mungu neema zake.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwatie nguvu Papa wetu F., Askofu wetu F. na Mapadre wote uliowaweka katika utumishi wako mtakatifu. Ee Bwana.

2. Pamoja na Raisi wetu kuwa huru kwa watu wote, umjalie roho ya ujasiri, apate kuwa hali zote kwa watu wote; ili afanye mambo yote kwa ajili ya manufaa ya wote. Ee Bwana.

3. Uwaongoe wazushi, wapinga dini na wote wenye mwenendo mbaya wa maisha, wapate kuishi kadiri ya kweli yako. Ee Bwana.

4. Uamshe ndani ya wanafunzi wote ari ya kutoridhika na vyeti tu, bali wajiandae kuhitimu vizuri kitaaluma na kimaadili, ili wasiwe viongozi vipofu. Ee Bwana.

5. Uwapokee ndugu zetu marehemu na kuwapa rehema na amani ya kudumu huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tuache unafiki, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.